Happy Lazaro, Arusha

Arusha .MBUNGE wa bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka nchini Ruanda ,Fatuma Ndangiza ametoa wito kwa nchi wanachama kuharakisha hatua za kisheria na kisera zitakazolinda haki za watu wenye ulemavu.

Aidha amesema kuwa, licha ya nchi hizo kusaini itifaki zinazohusu haki zao, bado mazingira mengi ya kijamii na huduma za umma hayajakidhi mahitaji yao.

Ndangiza ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari katika bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki .

Ndangiza amesema kuwa , wabunge walijadili hoja mbalimbali zikiwemo changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhakikisha wanapata haki na fursa sawa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Baadhi ya majengo ya umma, shule na hospitali katika nchi wanachama hayana miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo lifti na njia zinazowawezesha kuingia na kutumia huduma kwa urahisi hali hiyo inaendelea kuwa kikwazo kwa ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.”amesema Ndangiza 

Kutokana na changamoto hizo, Mbunge huyo ameitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka na kuimarisha sera zinazozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, huku wakisisitiza kuwa kusaini mikataba na itifaki pekee hakutoshi bila kuwepo kwa utekelezaji unaoonekana katika maisha ya kila siku ya wananchi

Aidha, mjadala huo uliibua hoja kuhusu kuchelewa kwa hatua za kukamilisha mchakato wa kisheria wa nyaraka zinazohusu haki za watu wenye ulemavu, ambapo wabunge waliwataka mawaziri wanaohusika na masuala ya Afrika Mashariki kuharakisha mchakato huo ili nchi wanachama ziweze kukamilisha hatua zinazohitajika na kuwezesha ulinzi wa haki hizo kuimarishwa kisheria

Mbali na masuala ya watu wenye ulemavu, Bunge hilo pia lilijadili maendeleo ya nguzo ya nne ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayohusu Shirikisho la Kisiasa, kufuatia ziara za kamati husika katika Tanzania na Somalia kwa lengo la kutathmini hatua zilizofikiwa kuelekea kuanzishwa kwa mfumo huo wa utawala wa pamoja.

Katika mjadala huo, wabunge walieleza kuwa pamoja na hatua zilizopigwa, bado kuna kazi ya kukamilisha mchakato wa kutengeneza Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki,hivyo nchi wanachama ambazo bado hazijawasilisha michango yao katika mchakato huo zilitakiwa kufanya hivyo ili kuwezesha hatua zinazofuata kuchukuliwa.

Wabunge hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha nguzo za awali za muungano wa kiuchumi, ambazo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Sarafu, ili kuondoa vikwazo vinavyozuia raia wa nchi wanachama kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii kwa uhuru zaidi ndani ya jumuiya hiyo.

Walieleza kuwa utekelezaji madhubuti wa nguzo hizo unapaswa kuwezesha wafanyabiashara kufanya biashara katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, wataalamu kutoa huduma nje ya nchi zao na wanafunzi kupata fursa za elimu katika nchi wanachama kwa masharti yanayozingatia makubaliano ya jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa hoja zilizotolewa, kuimarika kwa ushirikiano huo kutasaidia wananchi kunufaika moja kwa moja na fursa zinazotokana na Jumuiya ya Afrika Mashariki, jambo linaloweza kuongeza uungwaji mkono wa wananchi kwa hatua za kuimarisha ushirikiano wa kikanda na hatimaye kufikia Shirikisho la Kisiasa.