Na Silivia Amandius.
Mbunge Devotha Mburarugaba amejivunia fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa ya Specialty Coffee Association of Japan (SCAJ) 2026, yanayofanyika jijini Tokyo, nchini Japan, kuanzia Oktoba 14 hadi 16, mwaka huu. Katika maonesho hayo, pia anaiwakilisha kampuni ya Karagwe Estate Limited inayojihusisha na biashara ya kuuza kahawa nje ya nchi, iliyopo mkoani Kagera.
Mburarugaba ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi na dira yake ya maendeleo inayolenga kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo ambacho ni tegemeo la maisha ya Watanzania wengi.
Aidha, ametoa pongezi kwa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa kuratibu ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo, akieleza kuwa ni fursa muhimu kwa wazalishaji, wasafirishaji na wadau wengine wa kahawa kutangaza bidhaa zao, kukutana na wanunuzi wa kimataifa na kujenga mahusiano mapya ya kibiashara.
Amesema kupitia maonesho hayo amepata nafasi ya kukutana na wadau wa kahawa kutoka mataifa mbalimbali na kujifunza mwenendo wa soko la kimataifa, pamoja na mbinu zinazotumiwa na nchi nyingine kuongeza thamani ya kahawa kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje.
Ameeleza kuwa Tanzania inapaswa kuimarisha viwanda vya kuchakata kahawa ili kuongeza thamani ya zao hilo ndani ya nchi, badala ya kutegemea zaidi mauzo ya kahawa ghafi. Hatua hiyo, kwa mujibu wa maelezo yake, inaweza kuongeza manufaa kwa wakulima, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Mburarugaba amesisitiza kuwa ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya SCAJ 2026 ni fursa ya kukuza utambulisho wa kahawa ya Tanzania duniani, kufungua masoko mapya na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa lengo la kuongeza ushindani wa kahawa ya Tanzania katika soko la dunia.

