Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanaosimamia sekta ya utalii na wanyamapori wamekutana Oktoba 14, 2026 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha, kujadili hatua za kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukuza utalii, kuhifadhi rasilimali za asili na kuongeza ushindani wa EAC katika soko la utalii duniani.
Mkutano huo wa Makatibu Wakuu ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 13 wa Baraza la Kisekta la Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori unatarajiwa kufanyika Oktoba 15, 2026, ukilenga kupitia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo yaliyotolewa katika mikutano iliyopita, pamoja na kuweka mwelekeo wa kisera na kimkakati wa maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni uoanishaji wa sera za utalii, mifumo ya udhibiti, masharti ya utoaji wa leseni na viwango vya ubora wa huduma; kuimarisha juhudi za pamoja za kuitangaza EAC kama kituo kimoja cha utalii; pamoja na kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori na bioanuwai kwa matumizi endelevu ya rasilimali za utalii.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuendeleza na kusimamia rasilimali na vivutio vya utalii ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi, ajira na ustawi wa wananchi.
_“Nchi zetu zimejaaliwa vivutio vya kipekee vya utalii, ikiwemo hifadhi za taifa zinazotambulika kimataifa, mapori ya akiba ya wanyamapori, milima, fukwe, maziwa, mifumo ikolojia ya baharini, urithi wa utamaduni na vivutio mbalimbali vya kihistoria. Rasilimali hizi zinatuweka katika nafasi ya kipekee ya kushindana katika soko la utalii duniani”._ amesema Bw. Kadonya.
Ameeleza kuwa, licha ya utajiri huo wa vivutio, uwezo wa EAC kunufaika kikamilifu na sekta ya utalii unategemea ushirikiano madhubuti, sera na viwango vinavyolingana, utangazaji wa pamoja wa vivutio, miundombinu bora ya usafiri na uwekezaji endelevu.
Aidha, Bw. Kadonya amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa ukuaji wa sekta ya utalii unawanufaisha wananchi kwa upana, hususan wanawake, vijana, jamii za wenyeji na biashara ndogo na za kati, kwa kuwashirikisha katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo.
Mkutano huo unatarajiwa kuchangia katika kuimarisha uratibu wa sera na mikakati ya kikanda katika sekta ya utalii na usimamizi wa wanyamapori, kwa lengo la kuongeza ushindani wa EAC kama kituo kimoja cha utalii na kuhakikisha rasilimali zake zinahifadhiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Bw. Saleh Mohamed Juma, pamoja na watendaji waandamizi kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.

