Na Happy Lazaro, Arusha

Mwenyekiti wa wabunge wa bunge la EALA Tanzania ,ambaye ni Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki , Ansar Aboubakar Kachwamba, amesema wabunge wataharakisha mchakato wa kupitisha muswada wa haki za watu wenye ulemavu ili kuhakikisha kundi hilo linazingatiwa katika sera, mipango na miundombinu yote ya jumuiya hiyo.

Kachwamba ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari katika bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki linaloendelea jijini Arusha.

Amesema muswada huo ni muhimu kwa kuwa watu wenye ulemavu ni kundi maalumu linalotambuliwa na mifumo mbalimbali ya kimataifa, huku akisisitiza kuwa ulemavu ni hali inayoweza kumpata mtu yeyote wakati wowote wa maisha yake.

Ameongeza kuwa,haki za watu wenye ulemavu hazipaswi kuchukuliwa kama madai ya kundi hilo pekee, bali ni haki za msingi zinazopaswa kulindwa na kuheshimiwa na kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kumekuwa na ucheleweshaji katika kupitishwa kwa muswada huo, lakini sasa hatua za kuufanyia kazi zinatarajiwa kuendelea ili kuweka msingi wa kuhakikisha mahitaji ya watu wenye ulemavu yanazingatiwa katika shughuli zote za jumuiya.”amesema .

Aidha amefafanua kuwa ,muswada huo utasaidia kuhakikisha sera na miundombinu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inazingatia mahitaji maalumu ya watu wenye ulemavu, ikiwemo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa bila kukumbana na vikwazo visivyo vya lazima.

Ametoa mfano wa wabunge wenye ulemavu wanaosafiri kikazi, akisema wanahitaji wasaidizi wa kuwasaidia kutekeleza majukumu yao, jambo linalopaswa kuzingatiwa katika mipango ya usafiri na upatikanaji wa huduma nyingine zinazohitajika.

Amesema katika mazingira hayo, msaidizi wa mbunge mwenye ulemavu anahitaji pia kuwezeshwa kusafiri pamoja naye, pamoja na kuzingatiwa kwa mahitaji na nyenzo zinazohitajika ili kutoa msaada unaostahili.

Kachwamba amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawazuiwi kutekeleza majukumu yao kutokana na changamoto za kimazingira au mifumo ya huduma ambayo haijazingatia mahitaji yao.

Ameongeza kuwa kabla ya muswada huo kuwa sheria kamili, utapitia hatua zinazotakiwa za kibunge, ikiwemo kupokea na kuchambua maoni ya wadau ili kuhakikisha maudhui yake yanazingatia mahitaji halisi ya watu wenye ulemavu katika nchi wanachama.

“Wabunge wako tayari kuharakisha mchakato wa muswada huo utakapowasilishwa kwao, kwa lengo la kuupitisha kwa wakati na kuwezesha kuanza kwa utekelezaji wa masharti yatakayokubaliwa.”amesema Kachwamba.

Amesisitiza kuwa dhamira ya wabunge ni kuhakikisha muswada huo unakamilisha hatua zote zinazohitajika na kuwa sheria itakayosaidia kuimarisha ulinzi wa haki za watu wenye ulemavu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ameongeza kuwa, kupitishwa kwa muswada huo kutakuwa hatua muhimu katika kujenga jumuiya inayozingatia usawa, haki na ujumuishwaji, huku mahitaji ya watu wenye ulemavu yakipewa nafasi inayostahili katika maamuzi na mipango ya maendeleo ya kikanda.