Na Mwandishi Wetu,
Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, ameelekeza utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande pamoja na maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Serikali, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuendelea kufanya kaguzi katika maeneo ya Mahabusu na Magereza kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za kijinai ili kuendelea kuhakikisha hakuna msongamano wa Mahabusu na pamoja na kuwawezesha watuhumiwa wanaostahili kupata dhamana kwa mujibu wa sheria.
Waziri Ulega ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 13, 2026, wakati wa kikao cha kujitambulisha katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Njedengwa jijini Dodoma, ambapo amesisitiza umuhimu wa watendaji kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi na ufanisi ili kuimarisha upatikanaji wa haki nchini.
“Ni lazima tufanye kazi usiku na mchana kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande na maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Serikali, ili kuhakikisha kesi zinashughulikiwa na kufikishwa mahakamani kwa wakati, na watuhumiwa wanaostahili wanapata dhamana kwa mujibu wa sheria. Lengo letu ni kupunguza msongamano wa mahabusu na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati,” amesema Waziri Ulega.
Amesisitiza kuwa ukaguzi wa mahabusu unapaswa kufanyika kwa kasi na ufanisi nchini kote ili kubaini changamoto zinazochangia msongamano huo, kufuatilia hatua za kesi za watuhumiwa na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Aidha, ameelekeza kesi zinazostahili kufikishwa mahakamani ziwasilishwe kwa wakati, huku watuhumiwa wanaokidhi vigezo vya kupata dhamana wakipatiwa haki hiyo bila ucheleweshaji usio wa lazima, kwa kuzingatia masharti ya sheria husika.
Waziri Ulega ameeleza kuwa utekelezaji wa maelekezo hayo utasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu, kupunguza malalamiko ya wananchi na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ameeleza kufurahishwa na ongezeko la watendaji kutoka 630 hadi 1,200, akisisitiza kuwa ongezeko hilo linapaswa kuendana na kuimarika kwa kasi ya utendaji, weledi na ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili kuleta matokeo yanayotarajiwa katika mfumo wa utoaji haki nchini.
Vilevile, amevitaka vitengo vinavyohusika na elimu kwa umma kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya dhamana, ili waelewe vigezo na taratibu za kisheria zinazotumika katika utoaji wa dhamana na haki za watuhumiwa.
Amesema elimu hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao, kupunguza malalamiko yanayotokana na kutofahamu taratibu za kisheria na kuimarisha imani ya umma katika mfumo wa utoaji haki nchini.

