*Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo atembelea Banda la REA katika Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani
*Apongeza utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini
Tanga
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof. Peter Msofe, amepongeza jitihada za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Prof. Msofe ametoa pongezi hizo leo, Oktoba 13, 2026, alipotembelea Banda la REA katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika Viwanja vya Usagara, Tanga Mjini.
Akiwa bandani hapo, amepatiwa maelezo kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA, ikiwemo usambazaji wa umeme vijijini na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
REA inaendelea kutumia maadhimisho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu miradi na fursa za nishati, huku ikihamasisha matumizi ya nishati katika kuongeza tija ya uzalishaji, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, REA inawakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea banda lake ili kujifunza kuhusu huduma, miradi na fursa zinazopatikana katika sekta ya nishati vijijini.

