Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHULE ya sekondari Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambayo kwa miaka miwili imekuwa na ufaulu wa asilimia 100 kwa kitaifa kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne, wamejipanga kuhakikisha wanajiendeleza kitaaluma ili kuendeleza rekodi hiyo.
Mkuu wa shule ya sekondari Loiborsiret, mwalimu Fabian Amsi Doriye anaelezea mikakati hiyo kwenye mahafali ya 13 ya kidato cha nne ya shule hiyo.
Mwalimu Doriye amesema kwa miaka miwili mfululizo wanafunzi wa kidato cha pili na na nne wamekuwa na ufaulu wa kitaifa wa asilimia 100 katika mitihani yao na wataendeleza ufaulu huo.
Amesema mwaka huu wa 2026 wamewaanda ipasavyo wanafunzi 56 kutafanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, wakitarajia kiwango cha ufaulu kikiwa daraja la kwanza na la pili.
Amesema kuanzia mwaka 2024 amekuwa mkuu wa shule ya sekondari Loiborsiret na amekuwa na ushirikiano mkubwa na wanafunzi wa shule hiyo, walimu wenzake, wazazi na walezi katika kuhakikisha elimu bora inapatikana.
“Shule ya sekondari Loiborsiret imekuwa na ufaulu mzuri kitaifa hasa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne kwa ufaulu wa asilimia 100 na tunatarajia kuendeleza mafanikio hayo,” amesema mwalimu Doriye.
Hata hivyo, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyofanya kazi nzuri kupitia miradi mingi maendeleo ya shule hiyo ya sekondari Loiborsiret.
“Shule imepatiwa mradi wa majengo mawili ya maabara yenye thamani ya shilingi milioni 30 kwa fedha za EP4R madarasa na nyumba za walimu za kutosha,” amesema mwalimu Doriye.
Amesema wamepanga kununua photocopy mashine kupitia shirika lisilo la kiserikali la Namayana Foundation, wanamshukuru Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara, Yustina Rahhi ameahidi kuwachangia shilingi 500,000 na Meneja wa NMB Benki Simanjiro ameahidi kuwachangia shilingi 200,000.
Mgeni rasmi wa mahafali hayo Afisa Mtendaji wa Kata ya Loiborsiret, Charles Msangya amewataka wahitimu hao watumie muda mchache uliobaki kabla ya kufanya mitihani kwa kusoma kwa bidii ili kujikumbusha walichojifunza.
“Hatua mliyofikia kielimu msiridhike nayo kwani safari bado ni ndefu someni kwa bidii mwisho mpate vyeti, diploma, shahada na msiwasikilize wanaosema kuwa kuna watu wana fedha na hawajasoma, Mungu ndiye anayepanga, pia mtu mwenye elimu ni tofauti na asiyesoma,” amesema Msangya.
Mmoja wa wahitimu wa shule hiyo, Lena Nebuti amesema matarajio yake ya baadaye atakuwa mwanasheria kwani ana uhakika wa kufaulu mitihani yake kuanzia kidato cha nne.
