Wananchi wa Kijiji cha Uzi Kiswani, Mkoa wa Kusini Unguja, wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupiga marufuku uchimbaji wa mchanga katika fukwe za bahari, wakieleza kuwa shughuli hiyo inatishia usalama wa makazi yao na mustakabali wa kisiwa hicho.

Ombi hilo limetolewa leo, Oktoba 13, 2026, mbele ya Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Prof. Omar Fakih Hamad, wakati wa ziara yake ya kusikiliza changamoto na kero zinazowakabili wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Omar Suleiman alisema uchimbaji wa mchanga ufukweni umewaongezea hofu kutokana na kuongezeka kwa hatari ya maji ya bahari kuingia katika makazi yao. “Kwa kweli hii ni dalili ya kupoteza kisiwa, kwani maji ya bahari kila uchao yanakuja majumbani kwetu kutokana na uchimbaji wa mchanga ufukweni,” alisema Omar.

Wananchi hao walidai kuwa baadhi ya wachimbaji wanaendelea na shughuli hizo kwa baraka za viongozi wa Serikali, wakiwemo wanaohusishwa na kamati za Shehia. Mahadhi Abdulkheiry aliiomba Serikali kuchukua hatua za haraka, akionya kuwa uchimbaji huo unaweza kusababisha kisiwa cha Uzi kutoweka. “Kila unapopita, iwe ufukweni au kwenye makazi yetu, utaona mashimo ya kila aina ambayo yametuongezea hatari kwa watoto wetu na hata sisi wazee,” alisema Mahadhi.

Naye Marhumi Hemed Suleiman alisema hali hiyo inatia wasiwasi kuhusu usalama wa kisiwa na maisha ya wananchi, huku akitaka hatua zichukuliwe kabla madhara hayajawa makubwa zaidi. Wananchi hao pia wameitaka Serikali kupiga marufuku uvuvi unaotumia nyavu zinazoharibu mazingira ya baharini, wakieleza kuwa unachangia uharibifu wa matumbawe na samaki wachanga.

Mselemu Ali Fumu alisema uvuvi huo una madhara kwa viumbe wa baharini na rasilimali ambazo wananchi wanazitegemea kiuchumi. Aidha, wananchi hao walieleza wasiwasi kuhusu upatikanaji wa ajira za Serikali, wakidai kuwa baadhi ya vijana wazawa wa Uzi wanakosa fursa za ajira. Shamuni Husein Abdallah alisema vijana hao wanastahili kupata fursa sawa na wananchi wengine.

“Leo wageni ndio wanaonekana na kuthaminiwa kuliko sisi wazaliwa wa hapa. Inauma sana,” alisema Shamuni. Katika changamoto nyingine, Marhumi Hemed Suleiman alilalamikia uharibifu na wizi wa mazao ya wananchi, yakiwemo minazi, mananasi na mihogo, akidai kuwa baadhi ya wahalifu hukata mazao hayo na kuwalishia mifugo yao. Aliiomba Serikali kuongeza nguvu kukabiliana na vitendo hivyo ili kulinda mali za wananchi.

Kuhusu sekta ya utalii, wananchi hao walisisitiza umuhimu wa kuendeleza utalii unaozingatia sheria, mila na tamaduni za Wazanzibari, wakipinga vitendo wanavyodai vinakiuka maadili ya jamii. “Tusiwaache watalii wanaokwenda uchi na wanaotembeza pombe,” alisema Marhumi.

Is-haka Husein Abdallah, anayejitolea katika utunzaji wa mazingira kisiwani Uzi, alisema uharibifu wa mikoko, miti ya asili na fukwe unaweza kupunguza mvuto wa utalii na kuathiri uchumi wa eneo hilo. Alisema wananchi wamekuwa wakihifadhi miti ya asili ili kulinda mazingira na kuvutia watalii, akionya kuwa uharibifu wa rasilimali hizo unaweza kushusha thamani ya utalii wa Uzi.

Kwa upande wa kilimo cha mwani, wananchi hao wamewaomba wawakilishi wao kupaza sauti katika Baraza la Wawakilishi ili kuhakikisha bei ya zao hilo inaongezwa na kuendana na gharama za uzalishaji. Subira Abdul Bari aliiomba Serikali kuwapatia vifaa vya kisasa vitakavyowawezesha kulima katika maeneo yenye kina kirefu cha maji na kuongeza ubora wa uzalishaji. “Tupatiwe boti ambazo zitaweza kufika kina kikubwa cha maji,” alisema Subira.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Seif Hamad Suleiman, aliwaahidi wananchi hao kuwa atawasilisha kero zao katika Baraza la Wawakilishi ili zifanyiwe kazi na kutafutiwa ufumbuzi.

Akihitimisha ziara hiyo, Prof. Omar Fakih Hamad aliitaka Serikali kuangalia kwa karibu hali ya kisiwa cha Uzi, akisisitiza umuhimu wake katika uhifadhi wa mazingira na kukuza utalii. Aliwahimiza wananchi kushirikiana kulinda rasilimali za kisiwa hicho kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla, akionya kuwa uharibifu wa mazingira unaweza kuathiri wakazi wote.

“Kwa sababu wachimbaji wa mchanga na wanaokata miti ya asili wanatoka humu humu Uzi, nawaombeni sana mshirikiane kuulinda urithi wenu ambao ni muhimu kwa taifa,” alisema Prof. Omar, akisisitiza kuwa ni muhimu kulinda fukwe, mikoko, miti ya asili na rasilimali nyingine zinazokifanya kisiwa hicho kuwa na thamani ya kipekee.