Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)(kulia), akisalimiana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, walipokutana na kufanya mazungumzo wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok, nchini Thailand.
Na Benny Mwaipaja, Bangkok Thailand
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa uhusiano kati ya Tanzania na taasisi za fedha za kimataifa, ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), umeendelea kuimarika huku uchumi wa nchi ukionesha ukuaji wa kuridhisha.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo (12.10.2026) alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Ndiame Diop, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia inayofanyika Jijini Bangkok nchini Thailand.
Ameeleza kuwa robo ya kwanza ya mwaka huu imerekodi ukuaji wa uchumi wa asilimia 6.3, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ikilinganishwa na vipindi vilivyopita.
Aidha, amesema kuwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali na matumizi vimeenda vizuri, huku mfumuko wa bei ukiwa ndani ya viwango vilivyokubalika vya asilimia 3 hadi 5.
Kuhusu ushirikiano na Benki ya Dunia, Mhe. Balozi Omar amesema taasisi hiyo inafadhili miradi 33 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 8.8 katika sekta za viwanda, elimu, afya, kilimo na mifumo ya hifadhi ya jamii kama TASAF.
“Tunashirikiana kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati. Miradi hiyo ya kipaumbele ni pamoja na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa reli ya Kati (MGR) na Reli ya Kisasa (SGR), pamoja na miradi ya nishati inayolenga kuunganisha gridi ya Taifa na nchi jirani ya Zambia.
Kwa upande wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Mhe. Balozi Omar amebainisha kuwa Tanzania imemaliza programu iliyokuwa ikiendelea na sasa inafanya tathmini ya ndani ili kubaini mahitaji halisi kabla ya kuingia kwenye makubaliano mengine mapya.
Kati ya Mwaka 2022 na 2026, Tanzania ilipata ufadhili wa dola za Marekani bilioni 1.7 zilizotolewa na IMF ambapo kati ya fedha hizo, dola za Marekani bilioni 1.063 zilikuwa za Program ya Upatikanaji wa Mikopo Nafuu kwa ajili ya kuimarisha Uchumi ( ECF) na dola za Marekani milioni 636.5, zilikuwa na kutemeleza Program ya Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi ( RSF), iliyohitimishwa mwezi Agosti mwaka 2026
Mhe. Balozi Omar amesisitiza kuwa uhusiano na taasisi hizo ni mzuri, akitolea mfano wa ziara za viongozi wa ngazi ya juu wa Benki ya Dunia na IMF nchini Tanzania, ambao wameonyesha kuridhishwa na hatua za maendeleo zinazopigwa na Tanzania.
Kwa upande wa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Ndiame Diop, aliipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikia kiuchumi na kimaendeleo na kuahidi kuwa Banki yake itaenndelea kuwa mshirika wake muhimu kwa kufadhili miradi mbalimbali ya kimkakati ya Serikali na kikanda.
Alitaja miradi ya nishati, elimu, miundombinu ya reli hususan ushiroba wa kati, kusaidia kaya masikini kupitia TASAF, uendelezauji rasilimali watu pamoja na miradi ya kikanda, kwamba itaendelea kupewa fedha na Banki hiyo kulingana na mahitaji ya nchi.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)(Kushoto), ukiwa katika kikao na ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, walipokutana na kufanya mazungumzo wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok, nchini Thailand.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kushoto), akiagana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, walipokutana na kufanya mazungumzo wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok, nchini Thailand.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Bangkok, nchini Thailand)
