DENIS MLOWE, MUFINDI

MKUU wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Selekwa, amewahimiza wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, inayotarajiwa kufanyika Oktoba 17, 2026, katika Kijiji cha Kisada, Kata ya Bumilayinga.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Selekwa amesema Makamu wa Rais atatembelea na kuzindua Mradi Mkubwa wa Umeme wa Tanzania na Zambia (TAZA), ambao unatarajiwa kuwa chachu ya kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Amesema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa Wilaya ya Mufindi kwa kuwa utasaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kupunguza changamoto za nishati na kufungua fursa mpya kwa wawekezaji, hususan katika sekta ya viwanda.

“Mradi huu wa umeme utasaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Wilaya ya Mufindi kwa kupunguza matatizo ya kukatika kwa umeme. Pia, utasaidia kupanua wigo wa uwekezaji viwandani na kuchochea ukuaji wa soko la ajira kwa wakazi wa wilaya hii,” amesema Selekwa.

Aidha, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika Maonyesho ya Biashara na Uwekezaji ya Mufindi yatakayofanyika katika Uwanja wa Wambi kuanzia Oktoba 16 hadi 23, 2026.

Amesema maonyesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, na yatakuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kuonesha bidhaa, huduma na bunifu mbalimbali.

Kwa mujibu wa Selekwa, maonyesho hayo yanalenga kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Mufindi, hususan katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvI na biashara ndogondogo, ambazo zina uwezo mkubwa wa kuchangia ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo.

Amesisitiza kuwa maonyesho hayo pia yatasaidia kuwaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji, kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa wilayani humo na kuwavutia wawekezaji wapya kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Selekwa amesema juhudi hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kukuza uchumi, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Hivyo, ametoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa hizo kushiriki kikamilifu katika ziara ya Makamu wa Rais na maonyesho ya biashara ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Mufindi.