Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ameipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa unaoendana na matumizi ya teknolojia mbalimbali za kisasa.

Mh. Mwinjuma ameyasema hayo leo tarehe 12/10/2026 mara baada ya kutembelea kwenye banda la TET katika maonesho ya vitabu ya kimataifa ya 31 Tanzania yaliyoanza kuanzia tarehe 10, Okotoba katika viwanja vya Makataba ya Taifa, Posta Dar es Salaam.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kufanya hasa katika utekelezaji wa mtaala uliboreshwa unaoendana na upatakinaji wa vitabu kwa wanafunzi nchini,” amesema Mhe. Mwinjuma.

Awali, Naibu Waziri huyo alipata nafasi ya kufungua maonesho hayo ambayo yatafanyika kwa siku tisa, huku yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wasio Serikali nje na ndani ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amewaomba wananchi na wadau wa elimu nchini kujitokeza kushiriki kwenye maonesho hayo ya vitabu na kupata fursa ya kununua vitabu vya kiada kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari nchini.

“Karibuni katika banda letu mnunue vitabu hapa kwa ajili ya watoto wenu vitakavowasaidia katika ujifunzaji wao shuleni na pia mtapata nafasi ya kufahamu masuala mbalimbali yakiwemo majukumu tunaoyafanya nchini, ”amesema Dkt. Komba.

Maonesho hayo yanashirikisha wadau mbalimbali nchini wanaojishughulisha na uzaaji na uchapaji wa vitabu, ambapo yameanza tarahe 10 hadi 18 mwezi Oktoba.