Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya UONGOZI imesema Jukwaa la Uongozi wa Wanawake litafanyika jijini Dar es Salaam kwa mara ya sita leo, Oktoba 12, 2026, likiwa na kaulimbiu inayohimiza kukuza na kudumisha uongozi wa wanawake kwa muda mrefu barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Taasisi ya UONGOZI, jukwaa hilo litajadili mikakati ya kukuza nafasi za wanawake katika uongozi na kuhakikisha wanadumu katika nafasi hizo kwa muda mrefu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa jukwaa hilo litahusisha kipengele kipya kinachotokana na utafiti unaoendelea kufanywa na taasisi hiyo kuhusu namna ya kudumisha uongozi wa wanawake kwa muda mrefu nchini Tanzania.
Mgeni rasmi katika jukwaa hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salum Mkuya, huku Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Ndege Qwaray, akitarajiwa kutoa salamu maalumu.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa hotuba kuu itatolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Java Foods ya Zambia, Bi. Monica Musonda.
Jukwaa hilo limeandaliwa chini ya Programu ya Uongozi wa Wanawake (WLP) ya Taasisi ya UONGOZI na linatarajiwa kuwakutanisha viongozi wa biashara na siasa, wasomi pamoja na wadau wa maendeleo kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika.
Pia, wanawake viongozi 100 waliochaguliwa kujiunga na makundi ya tisa na kumi ya programu hiyo wanatarajiwa kushiriki katika jukwaa hilo.
Taasisi ya UONGOZI imeeleza kuwa Programu ya Uongozi wa Wanawake inaendeshwa kwa ushirikiano na Shule ya Usimamizi ya Chuo Kikuu cha Yale nchini Marekani, kwa msaada wa Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya.
Programu hiyo ya miezi sita inalenga wanawake wa Kiafrika walio katika nafasi za uongozi wa ngazi za kati na za juu katika sekta mbalimbali, kwa kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kuwazuia kufikia nafasi za juu za uongozi katika maeneo yao ya kazi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakufunzi wa programu hiyo ni wataalamu wa masuala ya mabadiliko na uongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Taasisi ya UONGOZI imefafanua kuwa ushiriki katika jukwaa hilo utakuwa kwa mwaliko maalumu pekee.

