NA; MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amewataka viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuweka mifumo endelevu ya ukusanyaji na utunzaji wa taka, kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kuchukua hatua za kupunguza athari za mvua za El Niño.

Waziri Masauni amesema usafi wa jiji haupaswi kutegemea maagizo kutoka kwa viongozi wa juu, bali unapaswa kuwa sehemu ya utendaji wa kila siku wa taasisi na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira.

Amesema Dar es Salaam ni sura ya nchi, hivyo viongozi katika ngazi zote wana wajibu wa kuhakikisha jiji linakuwa safi na mazingira yanatunzwa wakati wote.

Waziri huyo ametoa kauli hiyo Oktoba 11, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za usafi na hatua zinazochukuliwa kutunza mazingira katika Mto Ng’ombe, uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Amesisitiza kuwa licha ya changamoto za upangaji wa makazi katika baadhi ya maeneo ya jiji, ni muhimu kuimarisha udhibiti wa utupaji holela wa taka na kuweka mifumo madhubuti ya ukusanyaji wake ili kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.

Mhe. Masauni amesema Ofisi ya Makamu wa Rais haitakubali kuona utekelezaji wa shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira ukisuasua, akizitaka taasisi, halmashauri pamoja na viongozi wa wilaya na mkoa kusimamia jukumu hilo kwa umakini na uwajibikaji.

Ameeleza kuwa taka hazipaswi kuonekana kama uchafu pekee, bali zinaweza kuwa chanzo cha uchumi na fursa za ajira kwa wananchi endapo zitakusanywa, kutunzwa na kuchakatwa kwa utaratibu unaofaa.

Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka husika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa taka ili kuwezesha matumizi yake yenye tija na kuongeza thamani badala ya kutupwa ovyo na kuhatarisha afya za wananchi pamoja na mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema wilaya hiyo inaendelea kutekeleza kampeni za kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira.

Mtambule amesema wananchi wanaoishi karibu na Mto Ng’ombe wameelekezwa kuondoka katika maeneo hayo ili kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua, huku zoezi la kubomoa nyumba katika maeneo husika likiwa limeanza kutekelezwa.

Ameongeza kuwa shughuli za ukusanyaji na utunzaji wa taka zinaendelea, sambamba na juhudi za mamlaka za wilaya kuhamasisha jamii kushiriki katika kulinda mazingira.

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama, huku hatua za kudhibiti uchafuzi na kupunguza athari za mvua zikiendelea kusimamiwa.