Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Oktoba 12, 2026

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Pwani (RAS), Richard Kayombo, amesisitiza umuhimu wa kuanza mapema maandalizi ya miundombinu ya shule za sekondari kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2028, kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari.

Akifunga mkutano wa uchaguzi mdogo wa kumchagua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa (KUT) wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kayombo amesema maandalizi ya madarasa na miundombinu mingine ya shule yanapaswa kupewa kipaumbele ili kukabiliana na mahitaji yatakayojitokeza mwaka huo.

Mabadiliko ya mfumo wa elimu yanatarajiwa kusababisha wanafunzi wa Darasa la Sita na Darasa la Saba kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2027 na kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa pamoja Januari 2028, hali inayohitaji maandalizi ya kutosha ya madarasa na huduma nyingine za elimu.

Aidha, Kayombo amewahimiza walimu wenye ulemavu kutoruhusu hali hiyo kuwakatisha tamaa katika kutekeleza majukumu yao, akisisitiza kuwa ulemavu haupaswi kuwa kikwazo cha kufikia malengo yao.

Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto zinazowakabili walimu, ikiwemo kuongeza ajira, kupandisha madaraja na kulipa stahiki zao, huku akisisitiza umuhimu wa kufuatilia madai na malalamiko ya walimu ambao bado hawajapata haki zao.

Kayombo amesema Chama cha Walimu Tanzania ni taasisi muhimu kutokana na mchango wa walimu katika kujenga Taifa kupitia maandalizi ya wataalamu na viongozi wa sekta mbalimbali.

“CWT ni chama kikubwa kinachotambulika, na kundi hili la walimu ni hazina katika Taifa kwa kuwa lina nafasi kubwa katika kujenga Taifa kutokana na mchango wao katika kuzalisha wataalamu na viongozi kwenye sekta mbalimbali,” amefafanua Kayombo.

Pamoja na hayo, amewaelekeza maofisa elimu kuhakikisha walimu wanatendewa haki katika upandishaji wa madaraja kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa.

Pia, amewataka walimu kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu namna ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Kwa upande wake, Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Suzan Shesha, amesema mkutano huo uliandaliwa kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa kumchagua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa (KUT).

Amesema katika uchaguzi huo, kura 37 zilipigwa, ambapo Mwita Magige aliibuka mshindi kwa kupata kura 20, huku Abdalrahmani Ahmadi akipata kura 16 na kura moja ikiharibika.

Shesha amesema Mkoa wa Pwani una jumla ya walimu 11,000, akimuomba Kayombo kusimamia uendeshaji wa mabaraza ya wafanyakazi kwa wakati ili kuimarisha mawasiliano, ushirikiano na utatuzi wa changamoto zinazowakabili walimu.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa aliyechaguliwa, Mwita Magige, ameshukuru kwa ushindi huo na kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa walimu, akiahidi kuwasilisha changamoto zao katika ngazi za juu ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka.