Na Mwandishi wetu, Simanjiro 

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya amewaahidi wakazi wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, kupambania shule zao zipate usajili wa bweni ili ziweze kuhudumiwa chakula na Serikali.

Ole Millya akizungumza kwenye mahafali ya kidato cha nne ya shule ya sekondari Emboreet, amesema anawaalika Dodoma, wazee 10 wa kimila (malaigwani) na wazee maarufu wa eneo hilo ili kuzungumzia suala hilo.

Amesema wazee hao wa kimila na watu wenye ushawishi wa wilaya hiyo pamoja naye watakutana na Waziri Mkuu Mwigilu Lameck Nchemba ili kuzungumzia changamoto hiyo.

Amesema asilimia 80 au 90 ya wanafunzi wanaosoma Simanjiro ni jamii ya wafugaji hivyo serikali inapaswa kuhudumia chakula kwenye shule zao.

“Shule nyingi za msingi na sekondari zipo mbali na makazi ya jamii hivyo zinapaswa kupata usajili wa bweni ili wanafunzi walale huko huko na kupata chakula,” amesema Ole Millya.

Mkuu wa shule ya sekondari Emboreet Aziza Rajabu Msengesi ameeleza kuwa shule kutosajiliwa kuwa shule ya bweni kwa kidato cha kwanza hadi cha nne kunasababisha wazazi wengi kushindwa kumudu kuchangia chakula.

“Jambo hilo linasababisha wazazi wengine kuwahamisha watoto wao na kuwapeleka wilaya jirani ya Monduli ambapo shule zote zinapata ruzuku ya chakula kutoka serikalini,” amesema 

Diwani wa Kata ya Emboreet, Yohana Shinini amemshukuru Ole Millya kwa namna mfuko wa jimbo ulivyochochea maendeleo katika eneo hilo.

“Kupitia mfuko wa jimbo tulipata milioni 83 tukaboresha madarasa ya shule na pia vikundi vyangu vimepata mkopo wa shilingi milioni 80 kupitia mapato ya ndani ya asilimia 10 ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” amesema Shinini.

Hata hivyo, amesema kuna changamoto ya miundombinu kwenye barabara ya Laitunyo kuna korongo na mvua za El Nino zitakapoanza jamii na itapata kero kufika Emboreet makao makuu ya kata.