Naibu katibu Mkuu Wizara wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Hussein Mohamed Omar ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Kigamboni.
Dkt. Omar ameleza kuridhishwa kwake baada ya kufanya ziara leo, tarehe 9 Oktoba 2026 katika mradi wa ujenzi wa chuo hicho unaotekelezwa katika eneo la Gezaulole, kata ya Somangila Mtaa wa Kizani, akiwa amembatana na baadhi ya viongozi kutoka Wizara hiyo.
“Kwa kuangalia madarasa, karakana na ujenzi unavyoendelea tunapata imani kwamba katika chuo hiki baadhi ya kozi zinaweza kuanza mwezi Novemba,” amesema Dkt. Omar
Aidha Dkt Omar ameitaka VETA kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unaleta faida za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo huku akisisitiza viongozi wa Halmashauri hasa baraza la madiwani kushirikishwa kwa kupatiwa taarifa kuhusu mradi wa ujenzi ili wawe mabalozi wazuri wa kuleta wanafunzi katika chuo hicho pindi mafunzo yatakapoanza rasmi.
Sambamba na hilo Dkt Omar ameshauri katika ujenzi unaondelea kuangalia jinsi ya kuweka miundombinu itakayowezesha uvunaji wa maji ya mvua ili kukabiliana na hali za ukame zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Eneo lingine la kutazama ni eneo la nishati kama vile matumizi ya feni, viyoyozi. Tuna majengo machache na bado tuna ujenzi wa majengo mengi hivyo tutazeme eneo hili na kufanya maboresha katika michoro iliyosalia ili kupunguza matumizi ya nisahti kwa yaliyosalia sambamba na kupanda miti katika maeneo ya wazi,” ameongeza Dkt. Omar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA. Anthony Kasore Kasore amesema mradi wa ujenzi wa chuo hicho unatekelezwa na VETA kwa njia ya nguvu kazi ya ndani (Force Account), kupitia Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Dar-es-salaam huku msimaizi mkuu akiwa VETA Makoa Makuu.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza tarehe 26 Mei, 2023 ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa majengo 19 ambayo yalikadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.2 na awamu ya pili itahusisha ujenzi wa majengo 5 ambayo yamekadiriwa kugharimu shilingi bilioni 1.17 na kufanya jumla ya majengo kuwa 24. Kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 85.
“Chuo hiki kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 675 wa kozi za muda mrefu na wanafunzi 2000 wa mafunzo ya muda mfupi na kitakuwa na uwezo wa kulaza jumla ya wanafunzi 320 wa bweni wavulana 160 na wasichana 160,” amesema.
Amesema katika hatua ya ujenzi ilipofikia wananchi wanaweza kuanza kupata mafunzo huku ujenzi wa majengo yaliyosalia ukiendelea na kufafanua kuwa tayari mafunzo ya muda mfupi ya udereva wa awali yameanza kutolewa chuoni hapo.
Frank Mrupe ni mwanafunzi wa mafunzo ya awali ya udereva Chuo cha VETA Kigamboni anasema “tunapata kozi ya udereva hapa Kigamboni nashuruku tupo na walimu wetu darasani kwa mafunzo ya nadharia na hata kwenye mafunzo ya vitendo, nawasihi vijana wenzangu waje kujiunga mafunzo haya”

