NA SOPHIA KINGIMALI, DAR ES SALAAM
MAKAMU wa Kwanza wa Rais, Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman, amezitaka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi kutafsiri maamuzi yaliyofikiwa katika Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama (COP12) kuwa mipango, bajeti na hatua za kitaifa zitakazopimika ili kuboresha uhifadhi wa bahari na kuongeza manufaa ya uchumi wa buluu kwa wananchi.
Amesema mafanikio ya mkutano huo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya maamuzi yaliyopitishwa, bali kwa matokeo yatakayopatikana katika kulinda mifumo ya ikolojia ya bahari, kuimarisha maisha ya jamii za pwani na kujenga uchumi endelevu katika ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi.
Akizungumza leo Octoba 9,2026 wakati akifunga mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam, Othman amesema ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazovuka mipaka ya nchi, zikiwamo uchafuzi wa bahari, upotevu wa bioanuwai, athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga ya baharini.
Amesema bahari ya Hindi Magharibi ni rasilimali ya pamoja inayochangia usalama wa chakula, biashara, utalii, utamaduni na ajira kwa mamilioni ya watu, hivyo nchi wanachama zinapaswa kuimarisha juhudi za kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Othman amesema Zanzibar ina uzoefu katika kuunganisha uhifadhi wa bahari na ushirikishwaji wa jamii kupitia maeneo ya uhifadhi wa bahari, akitolea mfano eneo la uhifadhi la kilomita za mraba 470 ambalo limekuwa sehemu ya juhudi za kulinda mifumo ya ikolojia na kuimarisha usimamizi shirikishi kati ya serikali na wananchi.
Amesema kuanzishwa kwa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Novemba 2020 kulilenga kuimarisha uongozi wa sekta hiyo, huku juhudi nyingine zikihusisha kuwajengea uwezo wanajamii katika usimamizi wa mazingira ya baharini na maeneo oevu.
Amesisitiza kuwa uchumi wa buluu hauwezi kuwa endelevu iwapo utasababisha uharibifu wa rasilimali za asili au kuwaacha wananchi wanaotegemea bahari bila fursa za kiuchumi, akitaka maamuzi yajengwe katika sayansi, taasisi imara na fursa za haki kwa jamii.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Masauni, amesema mkutano huo umefanyika wakati muhimu ambapo Mkataba wa Nairobi unatimiza miaka 40 tangu ulipopitishwa mwaka 1985, ukiwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kulinda mazingira ya bahari na pwani.
Masauni amesema Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano huo pamoja na majukwaa ya biashara, vijana na wanawake yaliyolenga kutafuta fursa za uwekezaji katika uchumi wa buluu, hatua inayolenga kuunganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema nchi wanachama zimepitisha maamuzi muhimu yanayohusu utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa kuhusu bioanuwai ya bahari katika maeneo yaliyo nje ya mamlaka ya kitaifa, kupambana na uchafuzi wa plastiki baharini na kuimarisha upangaji wa matumizi ya maeneo ya bahari.
Aidha amezitaka nchi wanachama kuweka majukumu yanayoeleweka, muda maalumu wa utekelezaji na mifumo ya ushirikiano wa kifedha na kitaalamu ili kuhakikisha maamuzi hayo yanatekelezwa kwa ufanisi katika ngazi ya kitaifa na kikanda.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Elizabeth Mrema, amesema maamuzi yaliyopitishwa yanaweka mwelekeo mpya wa kuimarisha uchumi wa buluu kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na ustawi wa wananchi.
Mrema amesema maamuzi hayo yanajumuisha mikakati ya kikanda ya kukabiliana na uchafuzi wa plastiki, mipango ya kukabiliana na matukio ya uchafuzi wa bahari, uhifadhi wa mikoko na nyasi bahari pamoja na kuimarisha usimamizi wa mifumo ya ikolojia inayosaidia uvuvi na uhifadhi wa mazingira.
Amesema utekelezaji wake unahitaji kuongeza fedha za uhifadhi kupitia mifumo bunifu ya ufadhili, ikiwamo hati fungani za buluu, ufadhili wa pamoja kati ya sekta ya umma na binafsi na uwekezaji unaozingatia uendelevu wa mazingira.
Aidha Mrema amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanawake, vijana, wavuvi wadogo na jamii za pwani katika kufanya maamuzi na kusimamia rasilimali za bahari, akisema makundi hayo yana maarifa na mchango mkubwa katika kulinda rasilimali zinazotegemewa kwa maisha yao.
Amesema UNEP itaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kuimarisha utekelezaji wa maamuzi ya COP12, huku akizitaka serikali na wadau kuhakikisha ahadi zilizotolewa zinabadilika kuwa matokeo yanayoonekana kwa watu na mazingira.
Katika mkutano huo, nchi wanachama pia zimeelekeza nguvu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuunganisha thamani ya rasilimali za bahari katika mipango ya maendeleo na maamuzi ya uwekezaji, huku Mauritius ikichaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa 13 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi utakaofanyika mwaka 2028.
