📍ZANZIBAR
TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa washiriki takribani 800 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Mwaka wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika (APS-HRMnet), utakaofanyika Zanzibar kuanzia Novemba 10 hadi 13, mwaka huu.
Mkutano huo utafanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar ukiwa na lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma na kuharakisha mageuzi ya kimkakati yanayolenga kuongeza tija na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa kwa vyombo vya habari Oktoba 9, 2026, jumla ya washiriki 404 kutoka nchi 11 walikuwa wamejisajili na kuthibitisha kushiriki mkutano huo kufikia tarehe hiyo.
Nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Nigeria, Sierra Leone, Côte d’Ivoire, Ghana, Namibia, Lesotho na Zimbabwe.
Aidha, viongozi mbalimbali wa Afrika wamethibitisha kushiriki mkutano huo, wakiwamo Waziri na Katibu Mkuu wa Sierra Leone, Katibu Mkuu wa Somalia, Katibu Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Katibu Mkuu wa Guinea-Bissau, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu wa Kenya pamoja na Katibu Mkuu wa Zambia.
Mkutano huo unalenga pia kutoa fursa kwa wasimamizi wa rasilimaliwatu, viongozi na wataalamu wa sekta ya umma kubadilishana uzoefu na utaalamu utakaosaidia nchi za Afrika kuboresha mifumo ya usimamizi wa watumishi wa umma.
Katika mkutano huo, washiriki wanatarajiwa kujadili matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwamo Akili Unde (Artificial Intelligence), katika usimamizi wa rasilimaliwatu na utoaji wa huduma kwa umma.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Kuwezesha Mabadiliko ya Kimkakati ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Afrika kwa Kutumia Akili Unde.”
Mtandao wa APS-HRMnet unajumuisha nchi za Afrika zilizogawanyika katika kanda tano, ambazo ni Afrika Magharibi, Mashariki, Kati, Kaskazini na Kusini, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa rasilimaliwatu na kusaidia utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Tanzania, ikiwa nchi mwanachama wa mtandao huo, imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaowakutanisha viongozi, wanataaluma na wataalamu wenye dhamana ya kusimamia utumishi wa umma barani Afrika.
Mbali na majadiliano ya kitaalamu, mkutano huo unatarajiwa kutoa fursa kwa washiriki kujifunza tamaduni za Tanzania Bara na Visiwani, huku ukichangia kukuza ushirikiano na kuimarisha mahusiano kati ya nchi za Afrika.

