NA DENIS MLOWE ,MVOMERO
MKUU wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Richard Kasesela, amewataka watumishi wa umma wilayani humo kuzingatia nidhamu ya kazi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, akisisitiza kuwa hatasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kasesela aliyasema hayo mara baada ya kukabidhiwa ofisi, akieleza kuwa anahitaji kufanya kazi na watumishi wenye nidhamu, wanaozingatia maadili ya utumishi wa umma na walio tayari kutimiza wajibu wao kwa maslahi ya wananchi.
Alisema nidhamu ni msingi muhimu katika utendaji wa kazi na kwamba watumishi wanapaswa kutambua kuwa wamepewa dhamana ya kuwahudumia wananchi, hivyo ni lazima watekeleze majukumu yao kwa uadilifu na kujituma.
Alifafanua kuwa nidhamu ya kazi inahusisha kutimiza majukumu kwa wakati, kuheshimu taratibu na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma wanazostahili bila usumbufu usio wa lazima.
Kasesela alionya kuwa hatakuwa tayari kuvumilia uzembe na kutowajibika kwa watumishi, akieleza kuwa atatumia mifumo iliyopo ya usimamizi na malalamiko kutambua changamoto za kiutendaji na kuchukua hatua zinazostahili kwa mujibu wa taratibu.
Alisema anataka kujenga mazingira ambayo wananchi watapata huduma bora na kwa wakati, huku watumishi wakitekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
Aidha, aliwataka watumishi kutambua kuwa wananchi ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele katika utoaji wa huduma, akisisitiza umuhimu wa kuwaheshimu na kuwasikiliza wanapofika katika ofisi za Serikali kupata msaada.
Alieleza kuwa atafanya tathmini ya utendaji wa watumishi ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho, akisema lengo lake ni kuhakikisha Wilaya ya Mvomero inakuwa mfano wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kasesela alisema huduma kwa wateja ni eneo muhimu linalopaswa kupewa uzito na kila mtumishi, huku akisisitiza kuwa nidhamu, uwajibikaji na namna ya kuwahudumia wananchi vitakuwa miongoni mwa mambo atakayoyapa kipaumbele katika uongozi wake.
Katika hatua nyingine, aliwataka watumishi wa wilaya hiyo kutambua fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Mvomero na kuzitumia kama msingi wa kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Alisema wilaya hiyo ina fursa nyingi katika sekta za uzalishaji, zikiwamo kilimo na ufugaji, ambazo zinahitaji kutambuliwa, kuendelezwa na kuwekewa mikakati madhubuti ili kuongeza tija na kipato cha wananchi.
Aliongeza kuwa, kwa kufanya tathmini ya kina ya rasilimali na fursa zilizopo, Serikali inaweza kubaini maeneo mengine yenye uwezo wa kukuza utalii na kuvutia uwekezaji, hata yale ambayo hayajapewa uzito unaostahili.
Kasesela alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya watumishi wa umma, viongozi na wananchi ni muhimu katika kubaini fursa hizo na kuandaa mikakati itakayochochea maendeleo ya Mvomero na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla.
