Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema mkoa huo umepokea jumla ya Shilingi trilioni 1.65 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa fedha hizo ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta Tija.

Nyongo aliyasema hayo wakati akielezea maendeleo ya mkoa huo kwa mwaka huu wa fedha na masuala ya mapato.

Aidha alisema pamoja na fedha hizo za miradi ya maendeleo, Mkoa wa Pwani umejiwekea lengo la kukusanya Shilingi bilioni 112 katika mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo hadi kufikia Oktoba mwaka huu ulikuwa umekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 47.

Alisisitiza kuwa miradi ya maendeleo inapaswa kutekelezwa kulingana na fedha zilizotolewa, huku wakandarasi wakitakiwa kukamilisha kazi kwa wakati kwa kuzingatia masharti ya mikataba yao, ili wananchi waanze kupata huduma zilizokusudiwa bila ucheleweshaji usio wa lazima.

Kuhusu uwekezaji anasema Mkoa wa Pwani unaendelea kupokea wawekezaji kutokana na juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alifafanua kuwa mkoa huo una jumla ya viwanda 1,768, vikiwemo viwanda vikubwa 503, vya kati 248 na vidogo 1,017, pamoja na kongani 35 za viwanda, ikiwemo HWTZ SEZ.

Kuhusu upatikanaji wa nishati ya umeme, alieleza vijiji 409 vya mkoa huo vimefikiwa na huduma hiyo, huku usambazaji wa umeme katika vitongoji ukiendelea, ambapo mkoa unatarajia kufikia asilimia 95 ya vitongoji vilivyounganishwa na umeme ifikapo Desemba 2026.

Kuhusu changamoto za ardhi, Nyongo alibainisha kwamba mkoa unaendelea na mpango wa kuendesha kliniki za ardhi katika kila wilaya , kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuzingatia haki na sheria.

Fursa zilizopo katika sekta za kilimo, viwanda, madini, utalii, nishati na maji zinaendelea kuwa chachu mkoani hapo katika kukuza uchumi wa mkoa na kuongeza mapato, huku Nyongo akisisitiza usimamizi mzuri wa rasilimali na fedha za umma ni muhimu katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora, inakamilika kwa wakati na kutoa huduma zinazotarajiwa kwa wananchi.