KONGWA, DODOMA — 8 OKTOBA 2026. Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Bi. Lena Mwakisale, akiwa pamoja na viongozi wa Mamlaka hiyo, amefanya ziara katika Wilaya ya Kongwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja 2026.

Katika ziara hiyo, viongozi hao wametembelea taasisi za Serikali, taasisi binafsi pamoja na wananchi wanaonufaika na huduma ya maji bure, kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na DUWASA katika Kanda ya Kongwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi. Mwakisale amesema lengo la ziara hiyo ni kuwahamasisha wananchi kutumia fursa ya huduma ya maji safi na salama inayopatikana katika maeneo yao kwa kuunganisha maji majumbani.

Amesema DUWASA inaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi, huku ikitoa kipaumbele katika kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wateja katika upatikanaji wa maji safi na salama.

Aidha, viongozi hao wamepongeza hatua iliyopigwa na Ofisi ya Kanda ya Kongwa katika kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wenye uwezo tofauti kiuchumi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati wa ziara hiyo, jumla ya wazee 410 katika Kanda ya Kongwa wananufaika na huduma ya maji bila malipo, hatua inayolenga kuhakikisha huduma hiyo muhimu inawafikia pia wananchi wenye kipato cha chini na wanaoishi katika mazingira magumu.

Mpango huo unaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za DUWASA za kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja 2026, ambayo inalenga kuimarisha uhusiano kati ya DUWASA na wateja wake, kusikiliza maoni yao na kuboresha utoaji wa huduma.