Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Meya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Soko la Kisasa la Mnarani–Loliondo, linalotekelezwa kupitia Mpango wa TACTIC, huku akimtaka mkandarasi wa uzoaji taka kusafisha soko hilo na kuzibua mitaro yote ndani ya siku mbili.
Dkt. Mawazo ametoa maagizo hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa soko hilo, ambapo mradi umefikia asilimia 45 ya utekelezaji.
Ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo, akieleza kuwa soko hilo litakuwa la kisasa na lenye manufaa kwa wananchi wa Mnarani na maeneo ya jirani, ambapo amemtaka mkandarasi kuhakikisha linakamilika ifikapo Februari 2027 bila kuathiri ubora wa kazi.
Mradi huo unaotekelezwa na M/s Dimetoclasa Real Hope Limited una thamani ya Sh bilioni 19.83 na unahusisha ujenzi wa soko la kisasa, barabara za lami zenye urefu wa kilomita 4.8, bustani ya mapumziko na burudani pamoja na jengo la usimamizi wa mradi.
Akizungumza katika Soko la Loliondo, Dkt. Mawazo amesema mazingira ya soko hilo yanapaswa kuwa safi kwa kuwa linahudumia wafanyabiashara na wananchi kutoka ndani na nje ya Manispaa ya Kibaha.
Ameeleza mkandarasi wa uzoaji taka amekuwa akisuasua katika utekelezaji wa majukumu yake, hali iliyosababisha kuwepo kwa mlundikano wa taka unaoweza kuhatarisha afya za wafanyabiashara na wananchi, hivyo amemtaka kubadilika au Baraza la Madiwani kuangalia hatua zaidi, ikiwemo kusitisha mkataba.
Vilevile, amewataka wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kutunza mazingira kwa kutotupa taka kwenye mitaro na kuhakikisha wanakuwa na vifaa maalumu vya kuhifadhia taka.

