Msaidizi wa Usajili Mkuu, kutoka BRELA, Nassoro Mtavu, wakati akizungumza kwenye Tamasha la Arusha Artisan Festival linaloendelea katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha.

………..

Na Happy Lazaro,Arusha.

 WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wasanii na wabunifu nchini kuhakikisha kazi zao zinasajiliwa rasmi ili kulinda ubunifu wao na kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na kazi zao.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na
Msaidizi wa Usajili Mkuu, kutoka BRELA, Nassoro Mtavu, wakati akizungumza kwenye Tamasha la Arusha Artisan Festival linaloendelea katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha.

Mtavu amesema wamepata fursa ya kushiriki katika maonesho hayo yanayofanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 11, ambapo wamekutana na wasanii mbalimbali wakiwemo wachoraji, wachongaji na wabunifu wengine.

Amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umewawezesha kuzungumza moja kwa moja na wasanii na kubaini kiwango cha uelewa wao kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA, ikiwemo usajili wa kazi na urasimishaji wa biashara.

Mtavu amesema wamegundua kuwa baadhi ya wasanii hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kusajili kazi zao, hivyo wamewatumia fursa hiyo kuwaelimisha na kuwaelekeza namna ya kuhakikisha kazi wanazozibuni zinalindwa kisheria.

Ameongeza kuwa, baadhi ya washiriki walitaka kufahamu namna wanavyoweza kurasimisha shughuli zao kwa kusajili kampuni au majina ya biashara, ambapo BRELA imewapatia maelezo na kuwaelekeza hatua zinazopaswa kufuatwa.

“Tumeeleza na wameelewa, na kati yao wapo ambao wameahidi kufanya maamuzi ya kusajili ili wawe rasmi,” amesema Mtavu.

Aidha amefafanua kuwa,changamoto kubwa waliyoibaini katika mafunzo hayo ni matumizi ya mawakala au watu wa kati katika kufanya usajili, hali ambayo wakati mwingine huwafanya wamiliki wa biashara kushindwa kufikia akaunti zao baada ya usajili kukamilika.

Amesema BRELA imewaelimisha wananchi hao kuhusu umuhimu wa kutumia taarifa zao wenyewe wakati wa kutengeneza akaunti, jambo litakalowawezesha kuingia kwenye mifumo na kufanya mabadiliko mbalimbali pale yanapohitajika bila kutegemea watu wengine.

Ameongeza kuwa , elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa itawasaidia wamiliki wa biashara kuwa na udhibiti wa taarifa zao na huduma wanazopata kupitia mifumo ya BRELA, badala ya kuendelea kutegemea mawakala kwa kila hatua.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kufika katika banda la BRELA na kupata majibu ya moja kwa moja kutoka kwa watumishi wa taasisi hiyo, akisema kufanya hivyo kutawasaidia kupata ufafanuzi sahihi na kutatua changamoto zao kwa wakati.