NA SOPHIA KINGIMALI, DAR ES SALAAM

MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amezitaka Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa katika Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba huo (COP12) yanageuzwa kuwa hatua zinazotekelezeka, kugharamiwa na kupimika ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili Bahari ya Hindi ya Magharibi.

Akizungumza leo Octoba 8,2026 wakati wa ufunguzi wa COP12 katika Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Ndejembi aliyemwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Mkataba wa Nairobi una nafasi muhimu katika kuunganisha ahadi za kimataifa na hatua za kikanda za kulinda bahari na mazingira ya pwani.

Amesema utekelezaji wa maamuzi hayo unapaswa kuanzia katika ngazi za kitaifa kwa kutafsiri Mkataba, itifaki zake na maamuzi ya mikutano ya nchi wanachama kuwa sheria, taasisi zenye uwezo, bajeti na mifumo ya utoaji taarifa inayoweza kupimika.

Ndejembi amesema nchi wanachama zinapaswa pia kuimarisha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kurejesha mikoko, nyasi za baharini na miamba ya matumbawe, kukabiliana na ongezeko la tindikali baharini na kuongeza upatikanaji wa fedha kwa jamii za pwani zilizo katika hatari.

“Mabadiliko ya tabianchi ndiyo tishio kubwa zaidi kwa bahari yetu na jamii zetu za pwani. Lazima tutende kwa haraka na kwa nia kubwa ili kujenga ustahimilivu na kulinda mifumo ya ikolojia inayotutegemeza,” amesema.

Amesema hatua nyingine ni kupambana na uchafuzi wa bahari unaotokana na plastiki, kemikali na maji taka, akisisitiza umuhimu wa kutumia mbinu ya kushughulikia uchafuzi kuanzia chanzo hadi baharini pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na matukio makubwa ya uchafuzi unaovuka mipaka.

Ndejembi amesema ulinzi wa bioanuwai unapaswa kwenda sambamba na uwekezaji wa baharini unaowajibika, ambapo mipango ya matumizi ya maeneo ya bahari, tathmini za mifumo ya ikolojia na hifadhi zinazozingatia maeneo zitumike katika kufanya maamuzi kuhusu uvuvi, bandari, utalii, nishati na shughuli nyingine.

Aidha, amesema nchi wanachama zinapaswa kuwekeza katika sayansi, utafiti, akili mbandia (AI), ufuatiliaji, kushirikiana data na kujenga uwezo wa kitaasisi ili kuhakikisha maamuzi kuhusu mazingira ya bahari yanaongozwa na ushahidi wa kisayansi na yanaweza kuvutia fedha endelevu.

“Sayansi lazima iwe msingi wa maamuzi yetu. Lazima tuwekeze katika utafiti, akili mbandia (AI), ufuatiliaji, ujengaji wa uwezo, na kuhakikisha kuwa maarifa bora yanayopatikana yanasaidia sera na programu zetu,” amesema.

Amesema ushirikishwaji wa sekta binafsi, wanawake na vijana ni muhimu katika kulinda mazingira ya bahari na kuendeleza uchumi wa buluu, akieleza kuwa COP12 imeanzisha Jukwaa la Biashara, Jukwaa la Vijana na Ushiriki wa Wanawake, hatua aliyotaka iwe sehemu ya mikutano ijayo.

Ndejembi amesema Bahari ya Hindi ya Magharibi ina thamani ya zaidi ya dola bilioni 300 katika rasilimali na kuzalisha takriban dola bilioni 20.8 kila mwaka, huku huduma za mfumo wake wa ikolojia zikikadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 25 kwa mwaka na zaidi ya watu milioni 65 wakitegemea bahari hiyo moja kwa moja kwa chakula na riziki.

Kwa upande wa Tanzania, amesema bahari ni muhimu kwa chakula na ajira, biashara, utalii na urithi wa kitamaduni wa jamii za pwani, lakini faida hizo zinakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi, uvuvi haramu na usio endelevu, kupotea kwa makazi ya viumbe na maendeleo yasiyopangwa vizuri.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuph Masauni, amrsema Tanzania kupitia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 inalenga kutumia fursa za uchumi wa buluu kwa njia endelevu kupitia kuongeza thamani, uvumbuzi, uwekezaji na kujenga mnyororo imara wa thamani.

Naye Kaimu Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Elizabeth Mrema, amezitaka nchi wanachama kutumia COP12 kugeuza ahadi za kimataifa kuhusu mazingira kuwa hatua zinazotekelezeka katika Bahari ya Hindi ya Magharibi, akisema changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa viumbe hai na uchafuzi zinahitaji ushirikiano wa kikanda kwa kuwa haziwezi kutatuliwa na taifa moja.