Happy LMkurugenzi wa Shirika la ASPA, linalojihusisha na ustawi na ulinzi wa punda, Livingstone Masija akizungumza na waandishi wa habari jijini Arushaazaro,Arusha .
Arusha. Wadau wa ustawi wa wanyama wameitaka Serikali kuimarisha udhibiti wa biashara ya punda nchini, wakieleza kuwa mnyama huyo ana mchango mkubwa katika maisha ya wananchi, hususan kwenye maeneo ambayo hutegemea wanyama wa kazi katika shughuli za kila siku.
Mkurugenzi wa Shirika la ASPA, Livingstone Masija, amesema punda si mnyama wa kupuuzwa kwa kuwa amekuwa akisaidia familia katika usafirishaji wa mizigo na shughuli mbalimbali za uzalishaji, hivyo jamii inapaswa kutambua thamani yake na kuhakikisha anapatiwa huduma zinazostahili.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari Jijini Arusha, Masija amesema matumizi ya punda yamekuwa na manufaa makubwa kwa wanawake na watoto, ambao hutumia wanyama hao katika kusafirisha maji, kuni, mkaa na mazao kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Amesema changamoto kubwa inayohitaji kupewa kipaumbele ni kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa zinazotokana na punda katika baadhi ya masoko ya nje, hali ambayo imeongeza thamani ya ngozi na sehemu nyingine za mnyama huyo.
Kwa mujibu wa Masija, imani zilizopo katika baadhi ya jamii kwamba bidhaa zinazotokana na punda zina matumizi ya dawa za asili na vipodozi imekuwa moja ya sababu zinazochochea mahitaji ya wanyama hao, jambo linalohitaji udhibiti ili kuzuia unyonyaji na usafirishaji usiofuata taratibu.
Amesema changamoto nyingine ni usafirishaji wa punda kupitia njia zisizo rasmi, hali inayofanya kuwa vigumu kwa mamlaka kufuatilia mienendo ya wanyama hao na kubaini iwapo taratibu za kisheria zimezingatiwa.
Masija amesema ASPA imekuwa ikijikita katika kuwasaidia wanyama ambao mara nyingi hawapewi kipaumbele, akiwemo punda, mbwa na paka, kwa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapatia chakula, maji, chanjo, matibabu na makazi yanayofaa.
Ameeleza kuwa hatua zilizowahi kuchukuliwa na Serikali dhidi ya shughuli za viwanda vilivyokuwa vikijihusisha na biashara ya punda katika Dodoma na Geita zilisaidia kupunguza shinikizo kwa wanyama hao, ingawa bado kuna haja ya kuendelea kuwa macho dhidi ya usafirishaji usio halali.
Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu punda, akiwataka waandishi kutumia majukwaa yao kutoa elimu juu ya thamani ya mnyama huyo na madhara yanayotokana na biashara isiyofuata sheria.
Kwa upande wake, Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la Habari Tanzania, Grace Macha, amesema mafunzo hayo yamewapa waandishi uelewa mpana kuhusu changamoto za ustawi wa punda na namna ya kuwasilisha taarifa zinazoweza kusaidia jamii kuwahudumia wanyama hao kwa usahihi.
Macha amesema elimu hiyo ni muhimu kwa sababu waandishi wanaweza kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu mahitaji ya msingi ya punda, ikiwemo upatikanaji wa maji na chakula, matibabu pamoja na mazingira salama ya kuishi.
Naye Daktari wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Robert Buluba, amewakumbusha wafugaji na wafanyabiashara kuhakikisha shughuli zao za usafirishaji wa mifugo zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Buluba amesema uzingatiaji wa masharti hayo unasaidia mamlaka kudhibiti usafirishaji wa mifugo na kupunguza uwezekano wa wanyama kusafirishwa kinyume cha taratibu, huku wafanyabiashara wakiepuka kuchukuliwa hatua kutokana na ukiukwaji wa sheria.

