Na Mwandishi wetu, Mirerani 

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa, Fadhili Rajab Maganya ameipongeza kampuni ya Chusa Mining LTD, kwa kujenga wodi ya wanawake na watoto

kwenye kituo cha afya Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Maganya ambaye pia ni Mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa, ameeleza hayo kwenye ziara yake ya siku moja Wilayani Simanjiro ambapo pia alifika kwenye kituo hicho cha afya na kukagua ujenzi wa wodi hiyo.

Amesema kampuni ya Chusa Mining LTD, chini ya Mkurugenzi wake Joseph Damas Mwakipesile imefanya jambo kubwa kwa jamii ya eneo hilo kwa kujenga wodi hiyo ya wanawake na watoto.

“Suala la wachimbaji kuwajibika kwa jamii (CSR) limekwenda sehemu husika kwani Chusa Mining LTD mngeweza kutengeneza bonanza la michezo ila mmegusa jamii katika sekta muhimu ya afya,” amesema Maganya

Amezungumzia pia gharama zilizotumika katika ujenzi huo kwani thamani ya fedha shilingi milioni 230 za ujenzi wake zinaendana na ubora wa jengo hilo.

“Gharama za ujenzi tumeona ni za kawaida na thamani ya fedha inaonekana kwenye jengo, siyo kama sehemu nyingine gharama unaambiwa ni shilingi milioni 80 ambayo haiendani nayo,” amesema Maganya.

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani, Dkt Namnyaki Lukumay akisoma taarifa ya ujenzi huo amesema jengo hilo linahusisha wodi ya wanawake, watoto na ofisi za madaktari.

Dkt Lukumay amesema hadi kukamilika kwake ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 230 fedha zilizogharimiwa na kampuni ya Chusa Mining LTD.