Na Victor Masangu,Kibaha
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt Mawazo Nicas ametoa muda wa siku saba kwa kiwanda cha kuchakata plastiki cha Cordy kilichopo kata ya Picha ya ndege kuhakikisha kinaweka mifumo mizuri ya mirereji ili kuondokana na changamoto sugu ya kutiririsha maji machafu.
Kiwanda hicho licha ya kupatiwa maelekezo ya muda mrefu na viongozi mbali mbali lakini bado kimeonekana kuwa ni kero kubwa kutokana na maji machafu kutoka kiwandani kwenda kwenye makazi ya watu.
Hayo yamegundulika baada ya mstahiki Meya huyo kufanya ziara ya kushtukiza katika eneo la kiwanda hicho na kukuta bado kinaendelea kutiririsha maji taka kwenye maeneo ya wananchi ambayo yanaenda kuathiri jamii na viumbe hai ikiwemo mifugo.
Ziara hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mtaa wa Picha ya Ndege kuhusu harufu kali na maji ya rangi ya nyeusi yanayotiririka mitaani na kuingia kwenye makazi yao na kuleta athari kwa jamii ikiwemo kubabuka pamoja na mifugo kufa inapokunywa maji hayo.
Mara baada ya kufika katika kiwanda hicho, Mstahiki Meya na timu yake kutoka Idara ya Mazingira walikuta bomba kubwa la siri pamoja na chemba likiwa limeelekezwa moja kwa moja kwenye mtaro unaopita kwenye makazi ya wananchi.
Dkt Nicas amesema Kiwanda hiki walishafika mara ya kwanza na kuwapa maelekezo ila wamekuwa ni wakaidi ukizingatia hili wanalofanya ni hatari Hii kwa afya ya jamii.
Amesema, kiwanda cha Cordy hakifuati sheria yoyote, hamna mfumo wa kuchuja maji taka (wastewater treatment), na hamna kibali cha Bonde cha kutiririsha maji hivyo amewapa siku saba kuweza kuhakikisha wanajenga mfumo wa maji taka na baada ya hapo mamlaka ya bonde waje kwa ajili ya kupewa kibali cha kutiririsha maji baada ya ya kuyatibu.
Aidha, Mstahiki Meya amewaagiza kabla ya kuchukuliwa hatua yoyote ya kisheria anawapatia hadi siku ya Jumapili ya tarehe 12/10/2026 kuweza kusafisha mtaro huo na atafika kwenye eneo hili kuangalia kama wametekeleza na isipofanyika hivyo watachukuliwa hatua kulingana na sheria ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Naye Afisa Mazingira Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Bryson Mpogoza amesema kiwanda hicho kilishapigwa faini na Baraza la Mazingira NEMC na waliahidi watatekeleza yale waliyoelekezwa ila imeonekana wamekuwa ni wakaidi.
Aidha mstahiki Meya amefafanua Manispaa itaangalia ni kwa namna gani wanahakikisha wanasimamia yale yote yaliyosemwa na Mstahiki Meya ikiwemo kusafisha maeneo wanayomwaga majitaka na kujenga mfumo wa uchujaji wa maji taka.
Mstahiki Meya amefanya pia ziara katika Kiwanda cha Keds na kuwapongeza kwa hatua nzuri waliyoifanya ya kutanua mtaro kwa urefu wa Mita 600 na amewataka kuendelea kurudisha jamii na kuongeza urefu wa upanuaji wa mtaro huo.
Nao baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Picha ya Ndege wamemshukuru Mstahiki Meya kufika kwani kiwanda cha Lake Oil kimekuwa kinamwaga kemikali kipindi mvua inanyesha ambapo msimamizi wa kiwanda hicho kilichopo kwenye ujenzi amesema kwa sasa hakuna kemikali bali hizo ni zile zilizokuwa awali hivyo ameagizwa kuweza kuchukua magari kwenda kuchimba mchanga huo uliojaa kemikali na kujaza mchanga mwingine mpya.


