Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Stephen Mbundi, akizungumza kwenye ziara hiyo ya Makamishna wa mamlaka za mapato katika ofisi za EAC jijini Arusha leo

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, akizungumza makao makuu ya jumuiya jijini Arusha

Na Happy Lazaro, Arusha 

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Stephen Mbundi, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa maandalizi mazuri ya Mkutano wa 46 wa CATA unaofanyika Arusha tarehe 5–9 Oktoba 2026, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza wakati wa ziara ya Makamishna wa Mamlaka za Mapato katika Ofisi za EAC iliyoongozwa na wenyeji, Mamlaka ya Mapato Tanzania chini ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, Balozi Mbundi amesema matumizi ya teknolojia, ubadilishanaji wa taarifa na uunganishaji wa mifumo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Wajumbe walipata fursa ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa Single Customs Territory na namna EAC inavyowezesha ushirikiano wa Forodha miongoni mwa Nchi Wanachama.

Ziara hiyo ni sehemu ya programu ya CATA 46 na imelenga kuwapatia Makamishna uzoefu kuhusu ushirikiano wa kikanda, uboreshaji wa mifumo ya Forodha na mageuzi ya kidijitali.

“Baada ya ziara hiyo, Makamishna walifanya kikao cha ndani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kuhusu uongozi na changamoto katika kusimamia mageuzi ya Mamlaka za Mapato.”

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, amesema mijadala ya Mkutano wa 46 wa CATA itakuwa chachu ya kuboresha zaidi huduma za kodi nchini.

Mwenda ameyasema hayo akiongoza ujumbe wa CATA ulipotembelea Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya programu ya mkutano huo unaofanyika tarehe 5–9 Oktoba 2026.

Mwenda amesema ziara hiyo imewapa Makamishna fursa ya kujifunza uzoefu wa EAC katika matumizi ya teknolojia, ubadilishanaji wa taarifa na uboreshaji wa mifumo ya Forodha, maeneo yanayochangia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kurahisisha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema TRA itaendelea kutumia maarifa na uzoefu unaopatikana kupitia mijadala ya CATA katika kuboresha huduma kwa walipakodi, kurahisisha ulipaji wa kodi na kuimarisha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Taifa.

Naye Rais wa Jumuiya ya madola ya Wakuu wa Mamlaka za Kodi (CATA) Abu Tariq Jamaluddin amesema matumizi ya teknolojia na ubunifu ni chachu ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa walipakodi.

Amesema ujumbe huo umevutiwa na ubunifu unaotumiwa katika eneo la Afrika Mashariki, hususan matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kurahisisha michakato ya kodi na huduma kwa walipakodi.

Pia ameipongeza Tanzania kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuendelea kuboresha mifumo rafiki kwa walipakodi na kuweka mazingira yanayorahisisha ulipaji wa kodi.

Amesisitiza kuwa Mamlaka za Mapato barani Afrika zinapaswa kuendelea kujiboresha katika matumizi ya teknolojia na ubunifu ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Amesema ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa Mamlaka za Mapato ni muhimu katika kuendeleza ubunifu, kuboresha huduma kwa walipakodi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.