Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

Oktoba 7,2026

MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imeeleza kuwa eneo maalum la uwekezaji linaloendelezwa Zinga, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, litafungua fursa kubwa za kiuchumi na ajira kwa vijana.

Mradi huo unatekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 9,800, huku awamu ya kwanza ikilenga kuendeleza maeneo ya kimkakati kwa ajili ya kongani za viwanda na teknolojia.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo linaloendelezwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema TISEZA inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuweka miundombinu muhimu ili kuwezesha shughuli za uzalishaji.

Nyongo amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Pwani kushirikiana na TISEZA katika kuwaandaa vijana ili waweze kunufaika na fursa zitakazotokana na uwekezaji huo, ikiwemo kuwawezesha kushiriki katika utekelezaji wa asilimia 10 ya fursa zinazotengwa kwa makundi hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi kutoka TISEZA, Anna Lyimo, amesema vijana wanapaswa kujiandaa kuchangamkia fursa za ajira zitakazopatikana katika sekta za uzalishaji, ufundi na uendeshaji wa viwanda.

Lyimo amesema kati ya viwanda 150 vinavyotarajiwa kuendelezwa katika eneo hilo, ambapo viwanda 25 vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza shughuli za kiuchumi na fursa za ajira katika eneo hilo.