Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Haroon Nyongo, amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha 191 Kisarawe, kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu, akisema uwekezaji huo utasaidia kukuza vipaji na kuwapa vijana mazingira bora ya kushiriki michezo.

Nyongo ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Kisarawe, ambapo alikagua uwanja huo na kuzitaka taasisi na mamlaka nyingine kuiga mfano huo kwa kuwekeza katika miundombinu ya michezo.

Amesema uwepo wa uwanja huo ni fursa kwa vijana kuendeleza vipaji vyao, huku pia ukiwa na uwezo wa kutumika kwa maandalizi na mazoezi ya timu kuelekea mashindano makubwa ya kimataifa, ikiwemo AFCON.

Amesema uwekezaji katika miundombinu ya michezo unapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa michezo ni sehemu muhimu ya kukuza vipaji, ajira na kuongeza ushiriki wa vijana katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka vijana kutumia fursa zinazotokana na uwepo wa miundombinu hiyo kwa bidii, nidhamu na kujituma, huku akisisitiza kuwa mafanikio katika michezo yanahitaji maandalizi, mazoezi na matumizi sahihi ya vipaji