Waziri wa Ujenzi Masanja Kadogosa akizungumza wakati alipotembelea miradi ya barabara jijini Arusha.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha Mhandisi Reginald Massawe akizungumza kwenye.ziara hiyo jijini Arusha
Happy Lazaro, Arusha
ARUSHA: Serikali imeongeza kasi ya ujenzi wa barabara mbalimbali jijini Arusha zinazolenga kuboresha miundombinu ya usafiri kuelekea mashindano ya AFCON, huku ikieleza kuwa miradi hiyo itaendelea kuwa na manufaa kwa wananchi hata baada ya mashindano hayo kumalizika.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo ya barabara leo jijini Arusha , Waziri wa Ujenzi Masanja Kadogosa amesema maandalizi ya miundombinu kwa ajili ya AFCON ni jukumu la Serikali nzima, hivyo wizara na taasisi zinazohusika zinapaswa kushirikiana kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Kadogosa amesema amefanya ziara hiyo ili kujionea kwa macho hali ya utekelezaji wa miradi, hatua inayomwezesha kupata taarifa za moja kwa moja kuhusu maendeleo na changamoto zinazohitaji hatua za Serikali.
“Barabara hizo hazijengwi kwa ajili ya AFCON pekee, bali ni uwekezaji wa muda mrefu utakaosaidia kuifungua Arusha, kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi, ikiwemo utalii na biashara”amesema Kadogosa.
“Nimekagua barabara hizi zote nimefurahishwa sana na kasi ya ujenzi wa barabara hizo kwani TANROADS wanafanya kazi nzuri sana na kwa kasi hii wanayoendelea nayo inaonyesha miradi hiyo itamalizika kwa wakati na kwa muda uliopangwa”amesema Kadogosa.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha Mhandisi Reginald Massawe amesema barabara ya Arusha–Kibaya–Kongwa ina urefu wa takribani kilomita 70, kuanzia Mbauda hadi Losinyai, mpakani mwa Arusha na Manyara, huku kilomita 13 zikitengwa kuwa sehemu ya kipaumbele katika maandalizi ya AFCON.
Amesema katika kilomita hizo 13, kipande cha kilomita 7.4 kinaanzia Mbauda hadi eneo kinapokutana na Arusha Bypass, huku ikijengwa kwa njia nne pamoja na barabara za huduma kila upande, na taa zitawekwa katika eneo lote linalopita mjini.
Mhandisi Massawe amesema kipande kingine cha takribani kilomita 5.6 ambacho kitaungana na Arusha Bypass na kinajengwa kwa njia mbili kutokana na kiwango cha magari kinachotarajiwa kutumia barabara hiyo.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa kilomita hizo 13 unafanywa na kampuni ya CCECC kutoka China kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 221, huku Serikali ikiwa tayari imelipa malipo ya awali ya takribani shilingi bilioni 21 na utekelezaji ukiwa umefikia asilimia 46.
Massawe amefafanua kuwa ,Serikali inalenga kukamilisha kipande hicho kabla ya kuanza kwa mashindano ya AFCON, huku mkandarasi akiendelea na kazi katika pande zote za mradi.
Aidha, amesema kuna mradi mwingine unaoanzia Arusha mjini katika eneo la Chuo cha Ufundi, kupitia Kona ya Nairobi kuelekea Uwanja wa Ndege wa Arusha, Kisongo, pamoja na maeneo mengine yanayounganisha mtandao wa barabara wenye urefu wa takribani kilomita 40.
Amesema mradi huo unajengwa kwa njia nne pamoja na njia mbili za huduma na unatekelezwa na kampuni ya China kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 77, huku malipo ya awali ya takribani shilingi bilioni 12 yakiwa yamefanyika.
Mhandisi Massawe amefafanua kuwa utekelezaji wa vipande vya kilometa 13 vya AFCON umefika asilimia 50.93 ambapo Wakala huo unaendelea kumsimamia mkandarasi kuongeza rasilimali, mitambo na nguvu kazi ili kuhakikisha vipande hivyo vinakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Amesema TANROADS imepewa jukumu la kujenga mtaro wa maji wenye urefu wa kilomita moja katika eneo la Sambasha kutokana na changamoto ya maji na mmomonyoko katika maeneo ya milimani, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika muda mfupi.
Kwa ujumla, mradi wa kilomita 18 unaotekelezwa katika maeneo hayo una thamani ya takribani shilingi bilioni 22, huku Serikali ikiendelea kushirikisha taasisi mbalimbali katika kutatua changamoto za maji, fidia na masuala mengine ili kuhakikisha miundombinu hiyo inakamilika kwa wakati.

