Hayawi hayawi sasa yamekuwa,hatimaye ujumbe wa mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) umetembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kushuhudia maajabu yaliyowaita.
Ujumbe huo umepokelewa na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana Abdul-Razaq Badru na kuwaeleza wajumbe hao kuwa Ngorongoro ni sehemu pekee duniani yenye ikolojia imara inayojumuisha uwepo wa wanyama aina zote, mimea, misitu, ndege, urithi na malikale.
Amesema kutokana na ikolojia yake serikali imeamua kulihifadhi eneo hilo na kutambulika kuwa ni maajabu duniani na hivyo kivutio bora cha utalii kinachovutia maelfu ya wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Baadhi ya wageni waliotembelea hifadhi hiyo wamesema kwamba kufika kwao Ngorongoro kumewapa fursa ya hisia na Ndoto kukutana na uhalisia na kufahamu maajabu ya ulimwengu hasa baada ya kushuhudia umbile ya Kreta ya Ngorongoro likiwa na wanyama zaidi ya 25,000 na spishi za ndege takribani 500.
Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani unaendelea jijini Arusha huku wageni kutoka mataifa mbalimbali wakifurahia utajiri wa urithi na utamaduni uliopo nchini.

