Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameliomba Bunge kuangalia upya sheria na taratibu za manunuzi ili kurahisisha upatikanaji wa fedha na vifaa vya miradi ya maendeleo, akisema ucheleweshaji wake unasababisha miradi kutokamilika kwa wakati.
Nyongo alisema hayo baada ya kukagua ujenzi wa Chuo cha VETA kinachojengwa katika Kata ya Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe, oktoba 6,2026 ambapo anasema moja ya changamoto zilizobainika ni kuchelewa kwa fedha na taratibu za manunuzi, hali inayosababisha ujenzi huo kusuasua.
Alisema kuna umuhimu wa kurahisisha mchakato wa manunuzi pale fedha za mradi zinapokuwa tayari ili utekelezaji uweze kwenda kwa kasi na miradi ikamilike kwa wakati.
Alieleza ujenzi wa chuo hicho ulitarajiwa kukamilika mwaka 2023, lakini umekumbwa na changamoto mbalimbali zilizosababisha kuchelewa, huku akipongeza kasi iliyopo kwa sasa.
Nyongo alifafanua kuwa,kuongezeka kwa viwanda Kisarawe kunahitaji kuwa na vijana wenye ujuzi wa ufundi, hivyo kukamilika kwa chuo hicho kutasaidia kuzalisha wataalamu watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira na viwanda vinavyoendelea kuanzishwa wilayani humo.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Saidi Masoud Kisiki, alisema mradi unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa majengo tisa.
“Ujenzi umefikia asilimia 68.3, huku kazi katika majengo manane ikiwa imesimama kusubiri vifaa ambavyo mchakato wa manunuzi yake unaendelea katika ngazi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST)”
Aliongeza kuwa mradi huo pia unakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji, barabara na umeme.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, alieleza tayari wamewasiliana na TARURA kuhusu changamoto ya barabara kuelekea chuoni hapo na kwamba hatua za kuishughulikia zinaendelea.
Alisema kukamilika kwa chuo hicho kutakuwa na manufaa makubwa kwa vijana wa Kisarawe kwa kuwa kitawapa fursa ya kupata elimu ya ufundi na ujuzi wa kuwawezesha kujiajiri.
Naye Mbunge wa Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, alieleza kwamba vyuo vya VETA vina nafasi muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana kwa kuwapatia elimu ya vitendo na ujuzi unaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa au kuajiri wengine.
Jafo alisema chuo hicho ni fursa kubwa kwa vijana wa Kisarawe kupata ujuzi katika fani mbalimbali na kutumia ujuzi huo kujikwamua kiuchumi.

