Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imepokea cheti cha shukrani katika hafla ya chakula cha jioni ya kufunga maonesho ya Tech & AI Expo Zanzibar 2026, yaliyowakutanisha wadau wa teknolojia, wabunifu na viongozi kujadili maendeleo ya uchumi wa kidijitali visiwani Zanzibar hivi karibuni.

Cheti hicho kilikabidhiwa na Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga, na kupokelewa na Afisa Mkuu wa Yas Business, Norman Kiondo. Waziri Soraga aliishukuru Yas kwa kuwa mdhamini mkuu wa tukio hilo.

Katika hafla hiyo, pia alikabidhi tuzo kwa washindi wa shindano la Hackathon na washiriki wa mijadala. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Soraga alisisitiza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukuza ubunifu, teknolojia na matumizi ya akili bandia ili kuendeleza uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake Bw. Norman Kiondo – Afisa Mkuu wa Kitengo cha Yas Business alisema “Tunashukuru kwa kutambuliwa kwa mchango wetu katika maonesho haya.

Yas itaendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma za kidijitali Zanzibar ili kuwasaidia wananchi na biashara kutumia teknolojia katika shughuli zao za kila siku. Tunaamini ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wabunifu ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya Zanzibar,” alisema Kiondo.