Na Sophia Kingimali
FURSA za uwekezaji katika uvuvi, ufugaji wa samaki, usindikaji wa mazao ya baharini, utalii wa bahari, usafirishaji wa majini, bandari, mafuta na gesi zimepewa msukumo kupitia Mkutano wa COP12 wa Mkataba wa Nairobi unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Octoba 6,2026 katika mkutano wa COP12 unaoendele jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni amesema mkutano huo unalenga kuibua miradi na programu za pamoja zitakazochochea uwekezaji katika uchumi wa buluu huku zikilinda mazingira ya Bahari ya Hindi.
Masauni amesema fursa hizo zinaweza kuongeza ajira na kipato kwa wananchi na serikali endapo zitatumika kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, akitolea mfano sekta ya utalii wa bahari ambayo inaweza kuongeza idadi ya wageni na manufaa ya kiuchumi.
Amesema ushiriki wa washirika wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali katika mkutano huo umefungua nafasi ya kutafuta rasilimali za kuwezesha utekelezaji wa miradi ya pamoja ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Aidha Masauni, Tanzania na nchi nyingine zinazopakana na Bahari ya Hindi zinakabiliwa na changamoto zinazofanana, hivyo kuna umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kuandaa miradi itakayolinda mazingira na kuongeza manufaa ya kiuchumi yatokanayo na bahari.
Amesema Tanzania imelenga kuhakikisha COP12 haiishii katika mijadala na maazimio, bali inazalisha miradi, programu na mikakati inayoweza kutekelezwa na kuleta matokeo kwa wananchi na nchi wanachama.
Masauni amesema mkutano huo umehudhuria zaidi ya watu 700 kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo wadau wa maendeleo, mazingira na sekta mbalimbali za uchumi.
Amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya mkutano huo, Tanzania imeandaa vikao maalumu kwa wanawake na vijana kwa lengo la kuwaongezea nafasi ya kushiriki katika shughuli za uchumi wa buluu, ubunifu na matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wa wanawake, Masauni amesema jukwaa hilo linatoa fursa ya kujenga ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kutengeneza mahusiano ya kibiashara, huku akisisitiza nafasi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi wa buluu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Muungano na Mazingira) Zanzibar, Khamis Juma Khamis amesema mshikamano wa nchi wanachama ni muhimu katika kulinda mazingira ya bahari kutokana na uchafuzi na uharibifu wa matumbawe unaotishia mazalia ya samaki na maisha ya jamii.
Amesema vita dhidi ya uchafuzi wa bahari vinahitaji sheria, ushirikiano na rasilimali za kutosha, pamoja na mifumo ya pamoja ya kurejesha mazingira yaliyoharibiwa na kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na rasilimali hizo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Dkt. Elizabeth Mrema amesema elimu kwa wananchi ni muhimu katika kulinda bahari, akisisitiza kuwa uchafu wa plastiki ni miongoni mwa vitisho vinavyoathiri viumbe vya baharini na maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali hizo.

