Waandishi nguli wa habari za michezo na burudani kutoka sehemu mbalimbali duniani, walioko nchini Tanzania kwa ziara ya kiutalii na kufuatilia maandalizi ya AFCON 2027, Oktoba 5, 2026 wamefika katika Hifadhi ya Ngorongoro na kushuhudia utajiri wa vivutio vya utalii nchini.

Katika ziara hiyo, waandishi hao wamejionea wanyamapori mbalimbali wakiwemo simba, faru, twiga na wengine, huku wakipata fursa ya kutembelea pia Makumbusho ya Binadamu wa Kale na kujifunza historia ya mwanadamu.

Waandishi hao wamesema ziara hiyo imewapa picha halisi ya Tanzania, wakisisitiza kuwa wageni watakaokuja nchini kwa ajili ya AFCON 2027 hawatapata fursa ya kufurahia mpira pekee, bali pia watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali na kujionea uzuri, historia na utamaduni wa Tanzania.

“Hii ndiyo Tanzania! Ukija kwa AFCON 2027, hutafurahia mpira tu—utapata pia nafasi ya kugundua maajabu ya Tanzania kama Ngorongoro.”