Mbunge wa Jimbo la Vunjo, *Mheshimiwa Enock Zadok Koola, amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa huduma ya maji katika maeneo ya vijijini, hususani katika maeneo ambayo bado yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
*Mheshimiwa Koola* alitoa kauli hiyo jana, *tarehe 5 Oktoba 2026*, wakati akishiriki hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Tisa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) pamoja na kuwaaga wajumbe wa Bodi ya Nane, hafla iliyohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maji, *Mhandisi Kundo Mathew.*
Katika hafla hiyo, *Mh. Koola* aliwapongeza wajumbe wapya wa Bodi ya Tisa kwa kuteuliwa na kuwataka kutazama kwa karibu mahitaji ya wananchi wa majimbo ya vijijini.
“Maeneo haya ni makubwa, mahitaji ya huduma ya maji ni makubwa, na kuyafikia kunahitaji mipango thabiti pamoja na rasilimali fedha za kutosha,” *alisema Mh. Koola.*
Aidha, *Mheshimiwa Koola* alisisitiza umuhimu wa *MUWSA* na *RUWASA* kushirikiana kwa karibu pale ambapo majukumu yao yanapokutana, akieleza kuwa taasisi zote mbili ni sehemu ya Serikali moja na kwamba wananchi wanahitaji kuona juhudi za pamoja katika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa ufanisi.
*Mheshimiwa Koola* pia alitoa shukrani kwa wajumbe wa *Bodi ya Nane ya MUWSA* kwa utumishi wao na mchango wao katika kipindi chao cha uongozi, huku akiwaombea *kila la heri wajumbe wa Bodi ya Tisa* katika kutekeleza jukumu hilo muhimu la kuhakikisha huduma bora za maji na usafi wa mazingira zinaendelea kuimarika.

