Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

WAUMINI wa Kanisa la Morovian Tanzania Jimbo la Misheni ya Ruvuma na Njombe Ushirika wa Songea,wamechanga zaidi ya Sh.milioni 26,260,600 katika harambee ya ujenzi wa kanisa jipya litakalokuwa na uwezo wa kuchukua watu 600 kwa wakati mmoja.

Mjumbe wa kamati ya ujenzi Wilfred Lazaro alisema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 8 ni fedha taslimu na Sh.milioni 17,469,600 zimeshawekwa benki na Sh.milioni 16 ni ahadi na malengo ni kukusanya Sh.milioni 50 ili kuwezesha kuanza kwa ujenzi huo.

Lazaro alisema,ujenzi wa kanisa hilo unahitajika kuanza haraka kwa sababu kanisa lililopo ni dogo lenye uwezo wa kuchukua waumini 150 kwa mara moja huku idadi ya wakristo imekuwa ikiongezeka kila siku hivyo kupelekea kuwa na uhitaji wa kujenga kanisa lingine kubwa.

Hata hivyo alisema,katika utekelezaji wa ujenzi huo changamoto kubwa ni namna ya kutimiza ndoto za ujenzi wa kanisa hilo na wanatamani kufikia angalau asilimia 10 ambayo ni Sh.milioni 50 ya hitaji ili kuanza kazi ya ujenzi huo.

“Pekee yetu hatuwezi kufikia lengo hilo bali tunahitaji msaada wako Babab Askofu pamoja na wadau mbalimbali wenye mapenzi mema na kazi ya Mungu,kwetu sisi kila mchango wa hali na mali kwa ajili ya kazi iliyoko mbele yetu tunaupa thamani kubwa sana”alisema.

Akizungumza na waumini waliojitokeza katika harambee hiyo Askofu wa Kanisa la Morovian Jimbo Kuu la Kusini Kennan Salum Panja,amewapongeza wakristo na waumini wa Kanisa la Morovian Jimbo la Ruvuma na Njombe kwa kujenga nyumba kwa ajili ya makazi ya Mchungaji na kuanzisha mradi wa ujenzi wa kanisa jipya.

“Sasa kuna mwamko mkubwa kwa waumini kujenga makazi ya viongozi wao pamoja na nyumba za ibada,natembea maeneo mengi ndani na nje ya Jimbo nashuhudia kuna manadiliko makubwa yanayofanywa na Wakristo katika kuboresha makazi ya viongozi wao wa Dini”alisema Askofu Panja.

Askofu Panja,ameipongeza kamati ya ujenzi chini ya mwenyekiti wake Imani Mkumbwa kusimamia na kukamilisha ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya Mchunguaji wa Kanisa hilo.

Amewasisitiza waumini kuendelea kushiriki,kujitolea nguvu na michango yao ili kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya kufikisha huduma za kiroho kwa watu wengi zaidi.

“Sasa tunatakiwa kutoka na kwenda mbali zaidi hasa maeneo ya vijijini kueneza neno la Mungu,tusiishie mjini tu kwani huko vijijini kuna watu wengine wanaohitaji kupata huduma za kiroho”alisisitiza Askofu Panja.

Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Kanisa hilo Iman Mkumbwa,amewataka wakristo kujitolea katika ujenzi wa nyumba za Mungu badala ya kutumia fedha kwenye mambo machafu kama uesharati na ulevi.

Mkumbwa,awashukuru waliofika kwenye harambee hiyo kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa kanisa tarajiwa na kuwaomba waliohaidi wakamilishe ahadi zao ili kazi ya ianze haraka.

“fedha ulizonazo unaweza kuziacha kwa kuwa hatujui saa wala siku ya kuondoka hapa dunia na mbaya zaidi watu watakaobaki wataanza kugombana,kwa hiyo ni vizuri ukatoa sehemu ya fedha na mali zako kujenga nyumba ya Mungu”alisema Mkumbwa.

Katika harambe hiyo Meneja wa Wakala wa maji usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga amechangia jumla ya Sh.milioni 5.2. kati ya hizo Sh.milioni 3 ni fedha taslimu na nyingine ni ahadi.