Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutoa kipaumbele kwa ajenda ya Afya ya Mama na Mtoto katika utekelezaji wa mipango yao ya kitaifa.

Rais Dkt. Samia amesema hayo leo tarehe 05 Oktoba, 2026, alipokutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Ikulu jijini Dar es Salaam,

Dkt. Tedros yupo nchini kwa ajili ya ziara ya kikazi, pamoja na kushiriki Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 05 hadi 09 Oktoba, 2026.

Akiwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Rais Dkt. Samia amesema ataendelea kushirikiana na viongozi wa nchi za Afrika kuimarisha afya ya uzazi, kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na ujauzito na kujifungua, pamoja na vifo vya watoto.

Amesisitiza kuwa Mpango Elekezi wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto, Mtoto Mchanga na Afya kwa Vijana unapaswa kutekelezwa kwa vitendo katika kila nchi, ikiwemo kuhakikisha wajawazito wanajifungulia katika vituo vya afya na watoto wanapata chanjo.

Aidha ameiomba WHO kuendelea kushirikiana na nchi za Afrika katika kutoa utaalamu na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali za kutekeleza mpango huo.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amelishukuru Shirika la Afya Duniani kwa msaada wake katika kuimarisha huduma za afya na uwezo wa Tanzania kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kwa nchi za Afrika katika kukabiliana na athari za milipuko ya magonjwa inayoweza kutokea wakati wa mvua za El Niño.

Viongozi hao pia wamejadili Mkataba wa Kimataifa wa Kukabiliana na Milipuko ya Magonjwa (WHO Pandemic Agreement), unaolenga kuimarisha ushirikiano wa nchi katika kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na majanga ya magonjwa. Rais Dkt. Samia ameeleza utayari wa Tanzania kushiriki katika juhudi hizo.

Kwa upande wake, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameupongeza uongozi wa Rais Dkt. Samia katika kutekeleza jukumu la Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, akisema juhudi zake zina umuhimu kwa Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla.

Aidha, amepongeza hatua zilizofikiwa na Tanzania katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.

Dkt. Tedros pia amepongeza mafanikio ya Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Afya ya Mama na Mtoto ulioandaliwa na Tanzania jijini New York, Marekani, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

“Tunaona fahari kwa kazi unayoifanya,” amesema Dkt. Tedros, akithibitisha utayari wa WHO kuendelea kuunga mkono juhudi za utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto, Mtoto Mchanga na Afya kwa Vijana barani Afrika.