Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linachunguza kifo cha mwanafunzi wa Darasa la Nne, mwenye umri wa miaka 11, anayesadikiwa kujinyonga kwa kutumia mkanda wa begi katika Shule ya Msingi Mwenge, Kata ya Kingolwira.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 5, 2026, na jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro tukio hilo lilitokea Oktoba 2, 2026, majira ya saa 1:00 usiku.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa mwanafunzi huyo alitumia mkanda wa begi alioufunga dirishani, akidaiwa kufanya hivyo kutokana na kutaka kununuliwa kalamu kwa ajili ya mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nne.
Aidha Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini mazingira na sababu za tukio hilo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
