Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), amefungua Mkutano wa Jukwaa la Wanawake wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), leo Oktoba 5, 2026, katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Mhe. Zungu amesema maendeleo yaliyopatikana katika kuongeza uwakilishi wa wanawake mabungeni yanatia moyo.
“Kwa mfano, nchini Tanzania, uwakilishi wa wanawake bungeni ni asilimia 39.5,” amesema.
Hata hivyo, amesema uwakilishi pekee hautoshi, hivyo mabunge wanachama wa IPU yanapaswa kuendelea kushughulikia vikwazo vinavyoathiri ushiriki madhubuti, uongozi na ushawishi wa wanawake katika michakato ya kisiasa na kibunge.
“Jukwaa hili linatoa fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kujadili masuala yanayolenga kuimarisha ushiriki wa wanawake katika maamuzi,” amesema.
Amesema wakati washiriki wanakutana Tanzania, wanapaswa kuthibitisha tena kuwa mabunge yanayoshirikisha makundi yote ni mabunge imara zaidi.
“Tunapokutana hapa Tanzania, hebu tuthibitishe tena kuwa mabunge yanayoshirikisha makundi yote ni mabunge imara zaidi,” amesema.
Mhe. Zungu amesema kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika nyanja ya kisiasa kunaimarisha taasisi za kidemokrasia na kuchangia katika utawala unaowakilisha vyema wananchi na kujali mahitaji yao.
Amewahimiza washiriki kutumia Jukwaa hilo kubadilishana uzoefu kwa uwazi, kujenga ushirikiano na kubainisha hatua madhubuti za kuchukua katika mabunge ya nchi wanachama.
“Majadiliano haya yanapaswa kutusaidia kutoka hatua ya ahadi hadi utekelezaji wa vitendo,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa kuondoa vikwazo vya kimfumo na kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa ya kushiriki katika maamuzi kunajenga imani katika taasisi na kufungua fursa za pamoja zinazohitajika ili kujenga dunia yenye haki na inayoshirikisha watu wote.
Ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unatarajiwa kufanyika baadaye leo.

