Kikosi cha Zanzibar Spice Boys, chenye wachezaji chipukizi 18 wenye umri wa miaka 12 na 13, leo alfajiri wameondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume kuelekea nchini Brazil kushiriki mashindano ya kimataifa ya soka la watoto ya PQCUPBRASIL 2026, yatakayofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 15 Oktoba 2026, Minas Gerais, Brazil.

Ujumbe huo umejumuisha makocha na timu ya ufundi, Mkuu wa Msafara pamoja na maafisa wa Serikali akiwemo Katibu Mtendaji Baraza la Michezo Said Marin. Balozi wa Heshima wa Brazil Mstaafu Mhe. Abdulsamad Abdulrahim, ndie Mkuu wa Msafara huo.

Zanzibar Spice Boys imepangwa katika Kundi A la U-13, pamoja na timu za Clube Minas Gerais, Soccer Pro Betim, Polo Novo Horizonte Rio Vermelho na Vitinho Soccer Itabira. 

PQCUPBRASIL 2026 inatarajiwa kushirikisha timu mbalimbali kutoka Brazil, Portugal, Argentina na mataifa mengine. 

Ushiriki wa Zanzibar Spice Boys unatarajiwa pia kuwa jukwaa la kuitangaza Zanzibar kupitia vipaji vya watoto, utamaduni, utalii na maendeleo ya michezo.

Wakati wakiwa uwanja wa ndege, kikosi hicho kitapata fursa ya kuagwa na Wazee, Ndugu na familia, viongozi wa Serikali, ikiwa ni sehemu ya kuwapa wachezaji moyo, nasaha na hamasa kabla ya kwenda kuiwakilisha Zanzibar nchini Brazil.