MOSHi – KILIMANJARO
Wataalam wa Sekta ya Maji wametakiwa kuhakikisha kazi za udabuaji zinazoendelea katika bonde la mto Rau zinamalizika kwa wakati.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Andrew Mathew (Mb) , amesema hayo wakati wa ukaguzi eneo la mradi wa udabuaji unaofanyika eneo la Kahe , Mwangalia Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa uratibu wa Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani.
Mhe. Kundo amesema utekelezaji wa shughuli za udabuaji zifanyike kwa haraka ili zoezi lisishindwe kuendelea kutokana na msimu wa mvua unaokuja.
Kazi hiyo imeonesha dhamira ya watendaji wa Sekta ya Maji ya kufanya kazi saa 24 katika kuimarisha huduma za maji.
Mhe Kundo amekagua chanzo cha maji cha kiwanda cha Kahawa na kupokea taarifa ya uboreshaji na upanuzi wa chanzo hicho.
Amesema ujenzi wa miradi ni jambo moja lakini uhifadhi wa vyanzo vya maji ni jambo jingine hivyo ni muhimu kuendelea kutoa elimu kuhusu uhifadhi,ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji na kuzingatia utaratibu wa mita 60.
Lengo la mradi kuboresha chanzo hicho ni kuongeza uzalishaji wa maji na kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama katika manispaa ya Moshi katika kata ya Kaloleni, Njoro na Miembeni.
Awamu ya kwanza ya mradi inathamani ya Shilingi milioni 70 na awamu ya pili Shilingi milioni 576.1 ambapo utanufaisha zaidi ya wakazi 22,283.

