Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Elimu Mkoa wa Atusha, Mwl. Dkt.Vicent Kayombo akizungumza kuhusu maandalizi hayo mkoani Arusha.
…………..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Jumla ya wanafunzi 62,079 mkoa wa Arusha wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Upimaji wa Kitaifa wa darasa la nne kwa mujibu wa mabadiliko ya ratiba, iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa kwa mwaka 2026.
Akizungumza na mwandishi wetu, Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Elimu Mkoa wa Atusha, Mwl. Dkt.Vicent Kayombo amesema kuwa, kati ya wanafunzi hao 62,079, wavulana ni 31,082 sawa na asilimia 50.1 na wasichana ni 30,997 sawa na asilimia 49.9.
Amefafanua kuwa, idadi hiyo ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya mitihani ni sawa na asilimia 98.2 ya wanafunzi 83,241 waliondikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2023 na kuongeza kuwa, mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili tarehe 05 na 06 Oktoba 2026, huku jumla ya shule za Msingi 900 zikiwa zimesajiliwa kufanya mitihani hiyo, ambapo shule 587 ni za mfumo wa Kiswahili na shule 313 ni za mfumo wa Kiingereza.
“Maandalizi yote yameshakamilika kwa mujibu wa Sheria, taratibu na kanuni za mitihani ya Taifa, wasimamizi wote wa mitihani wamepatiwa semina elekezi ya usimamizi wa mitihani hiyo, wanafunzi wameandaliwa vizuri kitaaluma, kiakili na kisaikolojia, zaidi tunawatakia kila la kheri katika mitihani yao”. amesema Dkt.Kayombo.
Hata hivyo amewasisitiza wanafunzi wote kuwa watulivu na kujiamini wakati wote mitihani huku akiwasisitiza wasimamizi kuzingatia taratibu za mitihani ya Taifa na kujiepusha na aina yotote ya vitendo vilivyo kinyume na taratibu, kwa kuwa kazi ya usimamizi imebeba dhamana ya maisha ya wanafunzi wanaowasimamia.
Dkt.Kayombo amewatakia mtihani mwema wanafunzi wote wanaofanya mtihani hiyo pamoja na kuwaombea kwa Mwenyenzi Mungu wapate ufaulu mzuri na hatimaye kufikia ndoto zao.
