Na.Sophia Kingimali.
Tanzania imeanza maandalizi ya kushiriki Mkutano wa COP12, ikilenga kuwasilisha na kusukuma ajenda za uhifadhi wa mazingira ya bahari na pwani, matumizi endelevu ya rasilimali za bahari pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia Maandalizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama Zinazotekeleza Mkataba wa Nairobi (COP 12), leo octoba 4,2926 Jijini Dar es salaam,Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano na Mazingira)Mhandisi Hamad Masauni amesema Serikali imeendelea kushirikisha wadau mbalimbali, wakiwamo Ofisi ya Makamu wa Rais, taasisi za Serikali, watafiti, mashirika, sekta binafsi na jamii, ili kuhakikisha Tanzania inaingia katika mkutano huo ikiwa na ajenda zinazolenga kulinda mazingira na kuongeza manufaa ya uchumi wa buluu.
Amesema COP12 ni fursa muhimu kwa Tanzania kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika uhifadhi wa bahari na pwani, ikiwamo kupata teknolojia, utafiti na rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mazingira na maendeleo endelevu.
Aidha Mhandisi Masauni amesema kuwa , Tanzania pia inalenga kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine, hususan za ukanda wa kusini, katika kukabiliana na changamoto zinazotishia mifumo ya ikolojia ya bahari na pwani.
Amesema mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuleta changamoto katika mazingira ya bahari, hivyo hatua za pamoja zinahitajika katika usimamizi wa rasilimali hizo na kuhakikisha matumizi yake hayaathiri uwezo wa vizazi vijavyo kunufaika nazo.
Aidha, Serikali imesisitiza umuhimu wa tafiti na matumizi ya teknolojia katika kutambua changamoto za mazingira ya bahari na kutafuta suluhisho zitakazowezesha rasilimali hizo kutumika kwa tija bila kuharibu mazingira.
Amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza uchumi wa buluu kupitia shughuli za uvuvi, utalii, biashara, huduma na shughuli nyingine zinazotegemea bahari, lakini fursa hizo zinapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia uhifadhi.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi unapaswa kuambatana na hatua za ndani za kulinda bahari, pwani na mifumo ya ikolojia inayotegemewa na mamilioni ya wananchi.
Katika hatua hiyo, Serikali imeendelea kuhimiza utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira, matumizi sahihi ya rasilimali za bahari, udhibiti wa uchafuzi na umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi.
Amesema wanafunzi na jamii zinapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu mazingira ili kujenga kizazi kitakachokuwa na uelewa wa umuhimu wa kulinda rasilimali za bahari na mazingira kwa ujumla.
Aidha, sekta binafsi na mashirika mbalimbali yameombwa kutumia fursa zinazotokana na uchumi wa buluu kwa kuwekeza katika shughuli endelevu, huku yakizingatia sheria na taratibu za uhifadhi wa mazingira.
Aidha waziri Masauni ametoa wito kwa Serikali, sekta binafsi, wanafunzi, mashirika, watafiti na jamii kwa ujumla kushirikiana katika maandalizi ya COP12 na utekelezaji wa ajenda zake, akisisitiza kuwa ulinzi wa bahari na mazingira ni jukumu la kila mmoja.

