Waongoza watalii nchini leo Oktoba 4, 2026 wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwaandaa kwa ajili ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5–9, 2026.

Kikao hicho kimeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, ambaye amewasisitiza waongoza watalii kuzingatia maadili, weledi na ubora wa huduma wakati wa kuwahudumia wageni watakaoshiriki mkutano huo.

Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wanatarajiwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, hivyo waongoza watalii wameelekezwa kuhakikisha wageni wanapata huduma bora na uzoefu wa kipekee wa utalii wa Tanzania.

Mkutano huo unatarajiwa kuiletea Arusha zaidi ya wageni 2,000, hatua inayotoa fursa kubwa ya kuitangaza Tanzania kama kituo muhimu cha utalii na mikutano ya kimataifa.