Mkurugenzi wa Taasisi ya MAPCO , Suzan John Pombe Magufuli akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha

Mkurugenzi wa shule hiyo ,Betty Allen Kweka akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha

Mkuu wa shule hiyo ,Raymund akisoma risala katika mahafali hayo

……………….
Na Happy Lazaro, Arusha
Mkurugenzi wa Taasisi ya MAPCO , Suzan John Pombe Magufuli, amewataka wazazi na walezi kutambua umuhimu wa kuwekeza katika elimu na malezi bora ya watoto, kwani misingi wanayojengewa wakiwa tangu wadogo ina nafasi kubwa katika kuwaandaa kuwa viongozi wenye maadili na uwezo wa kujisimamia katika jamii.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza katika mahafali ya tano ya darasa la awali katika shule ya awali na msingi ya Mount Carmel Sakina jijini Arusha .
Suzan Magufuli amewahimiza wazazi na walimu kuendelea kushirikiana katika malezi na elimu ya watoto ili kuwajengea msingi imara wa maisha yao ya baadaye
“Kwa namna ambavyo shule hii inapambana kuendeleza watoto wetu na kukuza vipaji.vyao na nimeona kuna ujenzi unaendelea namuunga mkono kwa kutoa mifuko 100 ya sementi na kiasi fulani cha hela kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa madarasa ili uweze kukamilika kwa wakati na watoto kuweza kutumia majengo hayo.”amesema Suzan Magufuli.
Amesema hatua ya watoto kuhitimu Pre-Unit na kujiandaa kuingia Darasa la Kwanza ni sehemu muhimu ya safari yao ya kielimu, hivyo wazazi hawapaswi kuona elimu ya awali kama hatua ndogo, bali wanapaswa kuipa uzito kwa kuwa ndiyo inayowajengea watoto msingi wa kujifunza na kukua.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwalea watoto katika misingi ya nidhamu, heshima na uwajibikaji, akieleza kuwa elimu yenye mafanikio haiishii darasani pekee, bali inapaswa kwenda sambamba na malezi yanayomsaidia mtoto kuwa mtu mwenye maadili na mchango chanya katika jamii.
Amepongeza uongozi wa shule ya Mount Carmel Sakina kwa kuendelea kuwaandaa watoto katika nyanja ya elimu na malezi, huku akiwataka wazazi kuendelea kushirikiana na shule ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunza, kukua na kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo ,Betty Allen Kweka, amesema shule hiyo imejikita katika kuwaandaa watoto kuwa viongozi wa baadaye kwa kuwajengea misingi ya uongozi, elimu na maadili tangu wakiwa katika hatua za awali za masomo.
Kweka amesema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma, huku wanafunzi wake wakifanya vizuri katika mitihani mbalimbali, akieleza kuwa lengo si kuwafundisha watoto kwa ajili ya kufaulu mitihani pekee, bali kuwajengea uwezo wa kuelewa, kujiamini na kutumia maarifa wanayopata katika maisha yao.
Amesema shule hiyo pia imekuwa ikisisitiza malezi yenye maadili, akieleza kuwa changamoto za migogoro katika baadhi ya familia zinaweza kuwaathiri watoto, hivyo wazazi wanapaswa kuvumiliana, kushirikiana na kujenga mazingira mazuri ya malezi ili watoto wakue katika msingi unaowapa utulivu na mwelekeo.
Aidha Kweka amewakaribisha wazazi kuwaleta watoto wao katika shule hiyo kwani inatoa ada zinazoweza kumudu na inapokea watoto kuanzia umri wa miaka mitatu, huku ikiwa na walimu na walezi wenye uzoefu wa kuhakikisha watoto wanapata elimu, malezi, chakula na mazingira salama wanapokuwa shuleni.
Amesema mahafali hayo ya darasa la awali ni mwanzo wa hatua nyingine ya kielimu kwa watoto hao kuelekea Darasa la Kwanza, huku akisisitiza kuwa shule hiyo itaendelea kuwaandaa watoto kwa misingi imara ili waweze kujiamini, kujisimamia na hatimaye kuwa viongozi bora katika familia, jamii na Taifa.
Naye Mkuu wa shule hiyo ,Raymund Rupia amesema shule hiyo imeweka mkazo katika kukuza vipaji vya wanafunzi kwa kuvisaka na kuvilea kuanzia ndani na nje ya shule, huku ikitoa masomo ya ziada ya Kifaransa, kompyuta, michezo na elimu ya kiroho yanayolenga kuwajenga wanafunzi katika maadili, ujasiri na uwezo wa kutumia lugha za kigeni.
“Shule yetu pia imekuwa ikifanya ziara za kielimu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dodoma, michoro ya mapango ya Kondoa-Irangi, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Culture Heritage, Ziwa Duluti na Uwanja wa Ndege wa Arusha, kwa lengo la kuwaongezea wanafunzi maarifa kupitia uzoefu wa moja kwa moja.”amesema Rupia.
Amefafanua kuwa , mkakati huo ni sehemu ya maandalizi ya kuwajenga wanafunzi kuwa viongozi bora wa Taifa hapo baadaye, huku shule ikianza kuona wanafunzi wakionesha vipaji na ndoto katika taaluma mbalimbali kama udaktari, ualimu, urubani na uongozi.
Aidha amesema pamoja na mafanikio hayo, shule inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vitano vya madarasa, ambapo vinne bado havijakamilika na kimoja hakijakamilika kabisa, hali inayofanya shule kuhitaji ushirikiano wa wadau katika kuboresha miundombinu.
Rupia amesema tangu kuanzishwa kwake, shule imeongezeka kutoka wanafunzi 13 na walimu wawili hadi kufikia wanafunzi 201, walimu 11 na wafanyakazi wengine wanane, akisema ongezeko hilo linaonesha mwitikio mkubwa wa jamii na kuongeza umuhimu wa kupanua miundombinu ili kutoa nafasi kwa watoto wengi zaidi.
