Na.Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua awamu ya tatu na ya mwisho ya udahili wa wanafunzi wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027, ikiwapa fursa nyingine waombaji ambao hawakufanikiwa kupata nafasi katika awamu mbili zilizopita kujiunga na vyuo vikuu nchini.
Hatua hiyo imekuja baada ya TCU kupokea maombi kutoka kwa baadhi ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu mbili zilizopita, pamoja na baadhi ya vyuo vikuu ambavyo bado vina nafasi za udahili kuomba kuongezewa muda ili viendelee na zoezi hilo.

Akizungumza Oktoba 3,2026 jijini Dodoma Katibu Mkuu wa TCU,Prof.Charles Kihampa,amesema kuwa, awamu hiyo itakuwa ya mwisho baada ya kukamilika kwa awamu mbili za awali za udahili kwa mwaka huo wa masomo.
Prof.Kihampa amesema kuwa awamu hiyo ya mwisho itaanza Oktoba 3 hadi 9, 2026, huku vyuo vikuu vikitakiwa kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi ili kuwawezesha waombaji kufanya uchaguzi na kutuma maombi kulingana na sifa walizonazo.
“Hatua hiyo imekuja baada ya TCU kupokea maombi kutoka kwa baadhi ya waombaji walioomba kuongezewa muda wa kutuma maombi ya udahili, pamoja na vyuo ambavyo bado vina nafasi katika baadhi ya programu na kuhitaji muda zaidi wa kuendelea na zoezi hilo.”amesema Prof.Kihampa
Amesema Tume inawashauri waombaji ambao hawakutuma maombi ya udahili katika awamu zilizopita au hawakufanikiwa kupata nafasi katika awamu ya pili kutumia fursa hiyo kuomba udahili katika vyuo wanavyovipenda, kwa kuzingatia sifa na vigezo vya programu husika.
Katika ratiba ya awamu hiyo, vyuo vitawasilisha TCU majina ya waombaji waliodahiliwa Oktoba 13 na 14, 2026, kabla ya kutangaza majina rasmi ya waliochaguliwa Oktoba 17 mwaka huu.
Aidha, waombaji watakaopata udahili katika vyuo zaidi ya kimoja watatakiwa kuthibitisha chuo kimoja watakachochagua kati ya Oktoba 17 na 19, 2026, ili kukamilisha taratibu za kujiunga na elimu ya juu.
Prof.Kihampa,amewataka waombaji waliodahiliwa katika vyuo zaidi ya kimoja katika awamu ya pili, pamoja na wale walioshindwa kuthibitisha udahili katika awamu ya kwanza, kukamilisha uthibitisho wao kuanzia Oktoba 3 hadi 19, 2026.
“Uthibitisho huo utafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri inayotumwa kupitia ujumbe mfupi wa simu au barua pepe zilizotumika wakati wa kuomba udahili. Waombaji ambao hawajapokea namba hizo wanashauriwa kuwasiliana na vyuo husika kupitia mifumo yao ya udahili ili kutumiwa namba hizo.”Amesisitiza
Hata hivyo amefafanua kuwa masuala yote yanayohusu udahili na uthibitisho wa nafasi yanapaswa kushughulikiwa moja kwa moja na vyuo husika, huku vyuo vikielekezwa kupokea changamoto za waombaji na kuzitatua kwa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa.
Tume imesisitiza umuhimu wa waombaji kufuatilia matangazo ya vyuo kuhusu programu zenye nafasi zilizobaki ili kutumia ipasavyo fursa hiyo ya mwisho ya kujiunga na elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
