*Umicore Hoboken yachakata malighafi zaidi ya 200 na kurejesha aina 17 za madini
Antwerp, Ubelgiji
Wito umetolewa kwa watanzanoa kuwawanaweza kupata fursa mpya za biashara kupitia ukusanyaji na utayarishaji wa vifaa chakavu vya kielektroniki vinavyoweza kuwa chanzo cha madini ya thamani.
Fursa hiyo ilibainishwa katika ziara ya ujumbe kutoka Tanzania katika Kiwanda cha Umicore Hoboken, nchini Ubelgiji, ambacho kinatumia teknolojia ya kisasa kuchakata mabaki ya viwandani na vifaa chakavu vya kielektroniki.
Akizungumza Oktoba 2, 2026, Mkuu wa Ugavi wa Malighafi za Urejelezaji wa Umicore Thierry Van Kerckhoven alisema kuwa, Watanzania wanaweza kushiriki katika mnyororo huo kwa kukusanya vifaa kama simu janja, betri na vifaa vingine vya kielektroniki vyenye madini.
Alisema, vifaa hivyo vinaweza kutayarishwa kwa ajili ya uchakataji na kuwezesha kurejeshwa kwa madini yaliyomo ndani yake.
“Fursa ipo katika kukusanya na kutayarisha vifaa chakavu kwa njia inayowezesha uchakataji na urejeshaji wa madini,” alisema Van Kerckhoven.
Van Kerckhoven aliongeza kuwa, Umicore Hoboken huchakata takribani tani 500,000 za mabaki ya viwandani na vifaa chakavu vya kielektroniki kwa mwaka, na kurejesha takribani aina 17 za madini, zikiwemo dhahabu, fedha, palladiumu na Platinamu ikiwa pamoja na uwezo wa kuchakata zaidi ya aina 200 za malighafi kutoka vyanzo mbalimbali, kwa kutumia teknolojia maalumu ya uchakataji wa madini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo alisema kuwa, Tanzania imepata nafasi ya kujifunza namna teknolojia ya kisasa inavyotumika kuongeza thamani na kurejesha madini kutoka kwenye bidhaa zilizotumika.
Aliongeza, uzoefu huo ni muhimu wakati Tanzania ikiendelea na juhudi za kuongeza thamani ya madini nchini.
“Kupitia kiwanda hiki tumejifunza kuhusu uchakataji na uongezaji thamani wa madini kwa kutumia teknolojia ya kisasa Tanzania kwa sasa inaendelea kutekeleza Sera ya Uongezaji Thamani, hivyo kupitia tulichokiona tutaenda kushirikiana na wenzetu,” alisema Mbibo.
Alieleza kuwa, Serikali itaendelea kutoa fursa kwa wataalamu wa Tanzania ikiwemo kujifunza teknolojia na uzoefu kutoka nchi nyingine ili kuongeza ujuzi na kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya madini.
Mbibo aliongeza kuwa, fursa nyigine ni kuongeza nafasi kwa vijana na wafanyabiashara nchini kuangalia uwezekano wa kushiriki katika biashara ya ukusanyaji na utayarishaji wa vifaa chakavu vya kielektroniki, ambavyo vinaweza kuwa chanzo cha malighafi yenye madini ya thamani.
Pamoja na kuongeza wigo wa fursa katika sekta ya madini, kutoka uchimbaji pekee hadi uchakataji, urejelezaji na uongezaji thamani wa madini.

