Na Victor Masangu, Pwani

Umoja wa wanawake (UWT) Mkoa wa Pwani katika kuadhimisha sherehe za wiki yao imeamua kuunga mkono juhudi za Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utunzaji wa mazingira kwa kuamua kufanya usafi wa mazingira katika baadhi ya nyumba pamoja na matendo ya huruma katika kituo cha afya Mkoani kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Katika sherehe za maadhimishioo hayo ambayo yameongozwa na Mwenyekiti wa umoja huo wa UWT Mkoa wa Pwani Zainabu Vullu ambaye pia ameweza kuambatana na na viongozi wengine mbali mbali wa ngazi ya Mkoa pamoja na viongozi wengine wa Wilaya pamoja na ngazi ya kata.

Mwenyekiti huyo pamoja na viongozi wengine wameweza kufanya matendo ya huruma kwa kuamua kwenda kutembelea wodi ya wazazi katika kituo cha afya Mkoani na kutoa mahitaji mabli mbali ya msingi kwa wakinamama wajawazito pamoja na wale ambao wamejifungua ikiwemo sabuni za kuogea, sabuni za kufulia, mafuta ya kupaka ,maji,juice, pamoja na vitu vingine mbali mbali.

“Kwa kweli mimi kama Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani nimefarijika sana kuungana na wanawake wenzetu katika siku hii muhimu ya wiki yetu ya wanawake na tumeamua maadhimisho yake kuyafanyia katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ambapo tumefanya matendo ya huruma katika kituo cha afya Mkaoni na kufanya usafi katika nyumba ya Katibu wa UWT Mkoa na nyumba ya Katibu wa UWT Wilaya kwa hiyo ni siku ambayo tumeweza kukutana na kuiadhimisha kwa furaha na upendo,”amebainisha Mwenyekiti Vullu.

Naye Katibu wa UWT Mkoa wa Pwani Aziza Omary hakusita kuwakumbusha wanawake kuhakikisha kwamba kwa sasa wanatakiwa wawe na upendo na na kuwa na mshikamano wa pamoja kwa kushirikiana katika mambo mbali mbali na kuachana kabisa na tabia ya kuendeleza makundi kwani changuzi mbali mbali tayari zimeshamalizika.

Kwa upande wake mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amesema kwamba kupitia maadhimisho ya wiki yao wamepata fursa hiyo ya kufanya usafi na matendo ya huruma na kuwahimiza wanawake hao kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuijenga jumuiya hiyo kuanzia ngazi za chini ikiwe sambamba na kuchapa kazi kwa bidii kuanzia ngazi za chini.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji kwa mgeni rasmi kuhusiana na mambo ambayo wameyafanya katika maadhimisho hayo Katibu wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Cesilia Ndaru amebainisha kwamba wameweza kufanya shughuli mbali mbali za kijamii kuanzia ngazi za matawi na mashina ikiwa pamoja na kuwahimiza wanawake kuweka mikakati endelevu ya kuongeza wanachama wapya lengo ikiwa ni kuimarisha jumuiya yao pamoja na chama.

Kwa upande wake Katibu wa kituo cha afya Mkoani Saimon Swai hakusita kuwashukuru kwa dhati viongozi wote wa UWT Mkoa wa Pwani pamoja na Wilaya kwa kuamua kutumia sherehe za maadhimisho ya wiki yao kwa ajili ya kwenda kutoa msaada wa mahitaji mbali mbali katika wodi ya wakinamama ambapo amesema sapoti ambayo wameitoa ni kubwa na itakwenda kusaidia mahitaji ya mama pamoja na mtoto.

Kilele cha sherehe za maadhimisho ya wiki ya Umoja wa wanawake wa UWT Mkoa wa Pwani ambao wameungana na viongozi wengine wa Wilaya yamekwenda sambamba kwa kufanya matendo ya huruma katika kituo cha Afya Mkoani pamoja na kuendesha zoezi la usafi katika nyumba ya Katibu wa UWT ngazi ya Mkoa pamoja na nyumba ya Katibu wa UWT ngazi ya Wilaya.